0
Displaying IMG_0570.JPGZAIDI ya wakazi elfu 30 wa kata mbili za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa mkoani Dodoma wanatarajia kuondokana na adha ya kukosa huduma ya afya karibu na maeneo yao baada ya Serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni mia 6 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kitakachengwa katika kitongoji cha Itongwi, kijiji cha Kalamba kata ya Kalamba.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji, ametembelea eneo hilo na kushuhudia wananchi wenye ari wakiwa wamejitolea nguvu zao kusafisha eneo ambalo kituo hiko kitajengwa ili kuwaondolea adha ya muda mrefu ya kufuata huduma za afya Kondoa mjini umbali wa zaidi ya kilometa 100.
Wakazi wa Kata za Kalamba na Haubi wilayani Kondoa mkoani Dodoma walijitokeza wakiwa na majembe, miundu, mapanga na mashoka kusafisha eneo la mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Kalamba kitakacho toa huduma ya mama na Mtoto, ambapo tayari, mawe, mchanga na kokoto vimekwisha pelekwa katika eneo la ujenzi.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dokta Ashatu Kijaji ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa Vijijini, amepongeza jitihada za wananchi hao kwa kujitolea nguvu zao kushiriki ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho majengo yake yatagharimu shilingi milioni 400.
Aidha, Dkt. Kijaji amesifu uamuzi wa  baadhi ya wanakijiji cha Kalamba wa kutoa maeneo yao zaidi ya ekari 6 bila kudai fidia ili kuwezesha kuanza kwa ujenzi wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika  ndani ya miezi mitatu ijayo.
Amesema kuwa kitendo hicho kinafaa kuigwa na watanzania wengine katika maeneo ambayo miradi ya kijamii inapita ili kuipunguzia serikali gharama za miradi na hivyo kuharakisha maendeleo ya wananchi.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma Dkt. Ikaji Rashid, alisema kuwa kituo hicho cha afya kitakuwa na majengo sita yakiwemo wodi ya wazazi,  jengo la upasuaji wa dharula wa mama wajawazito, jengo la kuhifadhia maiti na jengo la wagonjwa wa nje.
"Akina mama wajawazito watakao hitajika kufanyiwa upasuaji baada ya kubainika kuwa na changamoto ya uzazi watapatiwa huduma hapa hapa hivyo hakutakuwa na haja ya kukimbizwa mjini Kondoa hivyo wataepuka gharama na kuepuka kujifungulia majumbani" Alisisitiza Dkt. Rashid.
Alisema kuwa Serikali imetoa pia fedha kiasi cha shilingi milioni 220 kwa ajili ya kununua vifaa vitakavyotumika kutolea tiba baada ya ujenzi wa kituo hicho cha afya kukamilika.
Wakizungumza katika ziara hiyo ya kukagua eneo la ujenzi wa kituo hicho kipya cha afya Kalamba, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kondoa Bi. Hija Bakari Suru na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilayani Kondoa Alhaji Othman Gora wamewataka wakazi wa kata hizo mbili kujitolea kufanyakazi  ili mradi huo ukamilike kwa wakati.
Aidha, walisisitiza umuhimu wa kamati ya ujenzi kufanyakazi kwa bidii na kwa uadilifu ili malengo ya muda mrefu ya wananchi wa kata hizo la kupata huduma karibu na maeneo yao yaweze kufikiwa.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top