Kuna
kipande cha video kinasambaa mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa
Tanzania wanaoishi nchini Oman wamekusanyika ofisi ya Ubalozi
kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso na adhabu kali
wanazopata kutoka kwa mabosi wao.
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama
kipande hicho cha video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman
kwa madhumuni ya kujua usahihi wa jambo hilo.
Ubalozi
ulitoa ufafanuzi kuwa uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi
Oman na ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat
tarehe 23 Machi 2018. Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania
watakaopenda kushiriki wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania
takriban 200 walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi,
vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden Tulip.
Siku
ya mkutano ilipowadia, Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na
kusababisha ugumu wa kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi
yaliyofanywa yalilenga watu 300.
Kamati
ya maandalizi ilipoona ukumbi umejaa na watu walio nje ni weng mara
mbili zaidi ya watu waliokuwemo ndani ya ukumbi iliamua kufunga milango
na kuwaomba waliochelewa warejee nyumbani.
Uamuzi
huo haukuwafurahisha watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe
kwenye ukumbi wa mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa
kutokea vurugu kubwa.
Kutokana
na uhalisia huo, Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi
wa Watanzania wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano
huo uahirishwe na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi
na huduma nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.
Kutokana
na ufafanuzi huo, Wizara inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa
kipande hicho cha video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza
kuingia kwenye ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye
ofisi ya ubalozi wa Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na
mateso wanayoyapata.
Post a Comment
karibu kwa maoni