0
‘Vyama vya siasa vifuate taratibu kudai haki’ VYAMA vya siasa nchini vimetakiwa kufuata sheria na taratibu, zilizowekwa katika kudai haki katika masuala mbalimbali nchini ili kujiondoa katika matatizo, yanayoweza kujitokeza na kuhatarisha amani ya nchi.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama wakati ametoa ufafanuzi kuhusu hoja za wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria.
Hoja hizo zilijitokeza wakati wa kujadili taarifa ya Utekelezaji wa bajeti 2017/2018 na makadirio ya bajeti ya mwaka 2018/2019 ya mafungu ya taasisi, zinazosimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini mjini Dodoma.
“Kila raia anatakiwa kufuata na kutekeleza matakwa ya sheria na taratibu zilizowekwa na nchi ili kujiondoa katika matatizo yanayoweza kujitokeza kutokana na ukiukwaji wa sheria. Tujenge tabia ya utii wa sheria bila shuruti,” alisisitiza Waziri Mhagama.
Wakati wa majadiliano, ilibainika kuwa vipo baadhi ya vyama vya siasa, ambavyo vimeonesha wazi kuvilazimisha vyombo vya ulinzi na usalama, kuchukua hatua za kisheria, kisha vyama hivyo kurudi kuilaumu Serikali.
Aidha, Mhagama alifafanua kuwa hoja zilizohusisha mgogoro wa ruzuku na uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), maandamano, migogoro ya vyama vya siasa na hoja zote ambazo kuna kesi makahamani, kuachwa bila kujadiliwa kwa kuwa kuzijadili hoja hizo, kunaweza kuharibu mwenendo wa kesi.
Alishauri viachiwe vyombo husika, viendelee na taratibu zao kisheria. Alitoa wito kwa vyama vyote nchini, kufuata utaratibu wa Mahakama wa kukata rufaa, endapo vitaona haki haijatendeka.
Katika siku za hivi karibuni, kumeibuka tabia ya baadhi ya vyama vya siasa nchini, kushindwa kufuata sheria na taratibu za nchi na kusababisha vitendo vinavyoashiria uvunjifu wa amani.
Kwa kutambua umuhimu wa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, Asha Abdallah Juma alimpongeza Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa kazi nzuri anayoifanya ya kusimamia vyama vya siasa.
Pongezi hizo ziliungwa mkono na Waziri Mhagama, ambaye alisema kazi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inastahili pongezi na kutiwa moyo, maana si kazi nyepesi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top