0
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeshauriwa kuangalia uwezekano wa kutumia Teknolojia Mpya ya utengenezaji wa Bara bara kwa kutumia maadini maalum ambayo uchanganyaji  wake baadae unageuka kuwa  zege linaloweza kudumu kwa miaka mingi.
Ushauri huo umetolewa na Mratibu Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya utengenezaji wa Madini ya Margania kutoka Nchini Uturuki Bwana Ahmet Nesih ONAL  wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Ahmet  Nesih alisema Bara bara  mbali mbali zinazotengenezwa kwa  kutumia Maadini ya Margania zinaipunguzia Serikali  gharama Kubwa ya Fedha sambamba na matumizi mengi ya Vifaa wakati wa ujenzi wa miundombinu hiyo kwa ajili ya mawasiliano ya usafiri Mijini na Vijijini.
Mratibu Mkuu huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya utengenezaji wa Madini ya Margania alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Kampuni yake  umeshuhudia  ujenzi wa Bara bara nyingi katika maeneo mbali mbali Duniani zinazotumia mfumo wa Lami ambao unaweza kuepukwa kwa kupungua matumizi.
Alisema yapo baadhi ya Mataifa Ulimwenguni kama Qatar, Kuweit, Saudi Arabia na Iraq zilizoanza kutumia Teknolojia hiyo ya Madini ya Margania na kufanikiwa kupunguza  gharama kubwa.
Akitoa Shukrani zake  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Zanzibar ni miongoni mwa Nchi kadhaa Duniani zinazoendelea kujikwamua Kiuchumi kwa kujenga Miundombinu kadhaa ikiwemo ile bara bara ambayo hurahisisha mfumo wa Mawasiliano.
Balozi Seif  aliuomba Uongozi wa Kampuni hiyo ya utengenezaji wa Madini ya Margania ya Nchini Uturuki kuandaa Mpango Maalum utakaowawezesha Wahandisi wa Sekta ya Mawasiliano Zanzibar  kuiona Teknolojia  hiyo  na kuangalia mazingira ya Zanzibar iwapo inaweza kutumika.
Alisema licha ya juhudi kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya uimarishaji wa Miundombinu ya Bara bara lakini bado zipo baadhi ya Bara bara Mjini na Vijijini zinahitaji kuimarishwa  kwa kutumia Teknolojia itakayoziwezesha zidumu kwa kipindi kirefu.
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top