0
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye amezifungia rasmi timu za Simba na Yanga kutumia uwanja wa Taifa mpaka pale zitakaporuhusiwa tena na Serikali.
PAMBANO la watani wa jadi la Yanga na Simba, lililofanyika Jumamosi badala ya kuwa burudani, lilikuwa kero kutokana na mashabiki wanaodaiwa kuwa wa Simba, kuvunja viti baada ya wapinzani wao kufunga bao la kuongoza.
Mashabiki wa Simba walivunja viti 1,781 baada ya Amissi Tambwe kufunga bao, ambalo mashabiki hao, walidai kuwa mfungaji aliushika mpira kwa mkono kabla hajafunga bao hilo. Pia mashabiki walivunja mageti mawili ya kuingilia uwanjani, wakikaidi maelekezo yaliyowataka kuingia kwa kutumia mageti mengine, badala ya kung’ang’ania na kujazana sehemu moja tu ya kuingilia.
Serikali kupitia kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnaye ilitangaza juzi kuzizuia Simba na Yanga, kutumia Uwanja wa Taifa kwa muda usiojulikana hadi pale itakapotangazwa vinginevyo.
Kitendo kichofanywa na mashabiki hao ni cha kihuni na hakitakiwi kufumbiwa macho, kwani kinaharibu dhana ya michezo kuwa ni furaha na upendo kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu zinazoshindana.
Hii sio mara ya kwanza kwa mashabiki wa timu hizo maarufu, kukosa ustaarabu na kuamua kuvunja viti vya uwanjani, pale wanapohisi timu yao inafungwa au inaonewa na waamuzi, kwani huko nyuma walishawahi kufanya hivyo.
Uwanja wa Taifa umejengwa kwa gharama kubwa, tena kwa fedha za walipa kodi, baada ya wapenzi wa soka kulia kwa muda mrefu kuwa Tanzania haikuwa na uwanja mkubwa na wa kisasa wa michezo, kama zilivyo nchi nyingine zikiwemo zile za Kenya na Uganda, ambazo tayari zina viwanja vya kisasa vya Kasarani na Mandela au Namboole.
Ni jambo la kushangaza kuona mashabiki wanafanya uharibifu uwanjani, kwa kisingizio cha eti tu timu yao imefungwa, wakati wanajua kuwa mchezo huwa na matokeo matatu ya kufungwa, kushinda na kutoka sare.
Uharibifu wa mali za umma, umekuwa ukitokea mara kwa mara na wahusika wamekuwa wakiachwa bila kufanywa lolote. Hatua hiyo huzidisha vitendo hivyo vya kihuni, ambavyo pia vimekuwa vikililetea taifa hasara kubwa.
Klabu za Simba na Yanga zimeshindwa kuwaadhibu wanachama wao, kwani waleta vurugu wanajulikana, na hao hao ndio wanaoanzisha au kufanya vurugu kila siku, hivyo sio shida kuwabaini.
Tunapenda kulaani vitendo vyote vya vurugu vya kuvunja viti, mageti na vifaa vingine vya uwanjani wakati wa pambano hilo la watani wa jadi, kwani sio uungwana hata kidogo. Vitendo hivyo vinaondoa dhana halisi ya michezo kuwa ni upendo na urafiki. Baadhi ya waleta vurugu walinaswa na kamera wakati wakifanya vitendo hivyo vya kihuni.
Hivyo, tunaomba hao wawe mfano kwa wengine kwa kuchukuliwa hatua za kisheria ili vitendo hivyo visirudiwe tena hapa nchini.
Tanzania ni nchi ya amani, hivyo vitendo kama hivi vya kihuni, vinavyofanywa na mashabiki wachache, vinaharibu taswira nzima ya nchi yetu ya kupenda amani na mshikamano. Pamoja na ukongwe wa timu hizo mbili, lakini hadi leo timu hizo hazina viwanja vinavyoeleweka.
Hivyo, zinatakiwa kutumia vizuri mali za wengine zikiwemo za wananchi, kama ulivyo Uwanja wa Taifa. Ni matarajio yetu kuwa mbali na kuzuiwa kuutumia Uwanja huo wa Taifa, klabu hizo za Simba na Yanga, zitalipa kila kitu walichoharibu uwanjani hapo kuanzia viti, mageti na vitu vingine vyote.
Tunawakumbusha tena wapenzi wa soka kuwa michezo ni furaha na michezo ni upendo na sio vurugu na mambo mengine yasiyo ya kiungwana. Tunalaani vikali vurugu hizo, kwani kama mashabiki waliweza kuvunja viti na mageti, hapo baadaye wataumiza watazamaji wenzao, wachezaji na waamuzi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top