0
UFAULU kwa watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2016 umepanda kwa asilimia 2.52 kutoka asilimia 67.84 mwaka jana hadi asilimia 70.36, huku wavulana waking’ara katika matokeo hayo ambao wengi wametoka shule za Kanda ya Ziwa.
Aidha, watahiniwa 238 kutoka shule sita wamefutiwa matokeo yao baada ya kubainika wamefanya udanganyifu katika mtihani huo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk Charles Msonde ambaye alisema kati ya wanafunzi 10 bora waliofanya vizuri katika mtihani huo, msichana ni mmoja tu, Justina Gerald wa Shule ya Msingi ya Tusiime ya jijini Dar es Salaam.
Kati ya wanafunzi hao 10, watahiniwa saba wanatoka Shule ya Msingi Kwema iliyopo mkoani Shinyanga, wawili Tusiime na mmoja kutoka Kaizirege ya Bukoba mkoani Kagera. Dk Msonde alisema jumla ya watahiniwa 555,291 kati ya 789,479 waliofanya mtihani huo wamefaulu kwa kupata jumla ya alama 100 na zaidi kati ya alama 250.
“Idadi hii ya watahiniwa waliofaulu ni sawa na asilimia 70.36, kati ya hao wasichana ni 283,751 na wavulana 271,540. Mwaka 2015 ufaulu ulikuwa ni asilimia 67.84 kuwapo ongezeko la ufaulu kwa asilimia 2.52,” alisema Dk Msonde.
Watahiniwa 16,929 wamepata daraja A, watahiniwa 141,616 wamepata Daraja B, watahiniwa 396,746 wamepata daraja C, watahiniwa 212,072 wakipata daraja D na 21,872 wakipata daraja E . Dk Msonde alisema ufaulu katika masomo ya Sayansi na Maarifa ya Jamii umepanda kwa asilimia kati ya 4.06 na 14.76 ikilinganishwa na mwaka 2015 huku masomo ya Kiswahili, Hisabati na Kiingereza ufaulu umeshuka kwa asilimia kati ya 0.39 na 12.51 ukilinganisha na mwaka jana.
“Watahiniwa wamefaulu zaidi katika somo la Kiswahili ambalo ufaulu wake ni asilimia 76.81 na somo walilofaulu kwa kiwango cha chini ni Kiingereza lenye ufaulu wa asilimia 36.05,” alifafanua Dk Msonde.
Dk Msonde aliwataja watahiniwa waliofanya vizuri na shule zao kwenye mabano kuwa ni Japhet Stephano, Jamal Athuman na Enock Bundala (Kwema), Justina na Shabani Mavunde (Tusiime), Jacob Wagine, Isaac Isaac, Daniel Kitundu na Benjamin Benevenuto (Kwema) na Azad Ayatullah (Kaizirege).
Wasichana 10 bora ni Justina na Danielle Onditi (Tusiime), Linda Mtapima (Kaizirege), Cecilia Kenene (Mugini), Magdalena Deogratias (Rocken Hill), Asnath Lemanya (Tusiime), Fatuma Singili (Rocken Hill), Ashura Makoba (Kaizirege), Rachel Ntitu (Fountain of Joy) na Irene Mwijage (Atlas).
Wanafunzi wavulana 10 bora kitaifa, Japhet Stephano, Jamal Athuman na Enock Bundala (Kwema), Shabani Mavunde (Tusiime), Jacob Wagine, Isaac Isaac, Daniel Kitundu na Benjamin Benevenuto (Kwema), Azad Ayatullah (Kaizirege) na Benezeth Hango (Kwema).
Shule 10 bora ni Kwema na Rocken Hill (Shinyanga), Mugini (Mwanza), Fountain of Joy na Tusiime (Dar es Salaam), Mudio Islamic (Kilimanjaro), Atlas (Dar), St Achileus (Kagera), Giftskillfull (Dar) na Carmel (Morogoro).
Shule 10 ambazo hazikufanya vizuri ni Mgata, Kitengu, Lumba Chini (Morogoro), Zege na Kikole (Tanga), Magunga ya Morogoro, Nchinila ya Manyara, Mwabalebi (Simiyu) Ilorienito (Arusha) na Chohero ya Morogoro.
Mikoa 10 iliyoongoza kitaifa ni Geita, Katavi, Iringa, Dar es Salaam, Kagera, Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Njombe na Tabora wakati Halmashauri 10 bora ni Mpanda Manispaa, Geita Mji, Arusha Mji, Mafinga Mji, Chato, Mwanza Jiji, Moshi Mji, Mji Makambako, Ilemela na Hai.
Dk Msonde alizitaja shule 10 ambazo hazikufanya vizuri ni Mgata (Morogoro), Kitengu (Morogoro), Lumba Chini (Morogoro), Zege (Tanga), Kilole (Tanga), Magunga (Morogoro), Nchinila (Manyara), Mwabalebi (Simiyu), Ilorienito (Arusha) na Chohero (Morogoro).
Akizungumza na gazeti hili, mama mzazi wa mwanafunzi Justina ambaye ni msichana pekee katika wanafunzi 10 bora nchini akishika nafasi ya nne, Edna Majaliwa alisema wamefurahishwa na matokeo ya binti yao.
Majaliwa ambaye ni daktari wa watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alisema waliamini kuwa binti yao ambaye ni wa kwanza kuzaliwa kuwa angefanya vizuri, lakini si kwa kiasi hicho.
“Tulijua kuwa atafanya vizuri kutokana na juhudi zake za kupenda kujisomea, lakini si kwa kiasi hiki, kusema ukweli tumefurahi na tunampongeza sana binti yetu,” alisema Majaliwa.
Akijibu kama mwanawe ana dalili za kufuata nyayo zake za kuwa daktari, Majaliwa alisema: “Kusema ukweli anapenda biashara na masuala ya uchumi, labda abadilike mbele ya safari katika masomo yake.”
Naye Mwalimu Mkuu wa Tusiime, Philbert Simon alisema wamefarijika na matokeo ya shule yao ambayo yamechangiwa na juhudi za walimu katika kuwaandaa wanafunzi na ushirikiano na wazazi.
Aidha, kuhusu watahiniwa 238 ambao hawatapewa nafasi ya kurudia mtihani huo, Dk Msonde alisema Necta itajipanga kufanya ufuatiliaji wa makusudi kwa wanafunzi waliofaulu na kujiunga na kidato cha kwanza ili kujiridhisha na umahiri wao katika kumudu masomo ya sekondari, na endapo watabainika kufaulu kwa udanganyifu watafutiwa matokeo.
Alisema Necta pia imeshatoa taarifa za waliohusika na kushiriki udanganyifu kwa mamlaka zao za utumishi ili wachukuliwe hatua kwa mujibu na kanuni za utumishi wa umma na kusisitiza kuwa Baraza halitamvumilia mtumishi anayevunja kanuni na sheria za nchi kwa kuvuruga usimamizi wa mitihani ya taifa.
Akifafanua zaidi kuhusu udanganyifu huo, Dk Msonde alisema katika Shule ya Tumaini iliyoko Sengerema mkoani Mwanza, mmiliki wake, Jafari Mahunde aliiba mtihani, kuandaa majibu ambayo watahiniwa waliandika kwenye sare za shule na kuyatumia ndani ya chumba cha mtihani, udanganyifu hao ulifanyika kwa kusaidiwa na msimamizi ambaye ni Alex Singoye.
Alisema katika Shule ya Little Flower, Mwalimu Mkuu Cecilia Nyamoronga alishiriki kuiba mtihani, kuandaa majibu na kumpa Msimamizi Mkuu, Haruni Mumwi na Msimamizi Genipha Simon ili wawapatie watahiniwa ndani ya chumba cha mtihani wakati wakitekeleza udanganyifu huo, msimamizi mmoja alikamatwa na Ofisa wa Necta aliyekuwa akifuatilia.
Dk Msonde alisema katika Shule ya Mihamakumi, Sikonge mkoani Tabora, Mwalimu Mkuu Kaombwe Samweli na walimu Leonard Maleta, Andrew Michael, Gilbert Gervas na John Puna walikutwa na maofisa wa Takukuru na Kamati ya Mitihani ya Mkoa wakiwafanyia watahiniwa mtihani, mpango huo pia ulimshirikisha msimamizi Fatuma Selemani.
Alisema katika Shule la Qash wilayani Babati katika mkoa wa Manyara, Mwalimu Asha Mosha alijificha chooni kupokea maswali kutoka watahiniwa na kuandaa majibu na kumpatia mtahiniwa Najma Omari.
Alisema katika Shule ya St Getrude iliyopo Madaba mkoani Ruvuma, Mwalimu Mkuu Fridolina Mwalongo na walimu Michael Mwafongo, Leonard Huule, Samson Mwaijibe, January Hongilo, Alkano Kisakali na Theodate Hyere na wanafunzi walishiriki kufanya udanganyifu.
“Katika shule hii, walimu walijificha katika mabweni na kwenye nyumba ya mwalimu iliyopo karibu na chumba cha mtihani, watahiniwa waliomba ruhusa ya kwenda kujisaidia na kutoka na maswali kuwapelekea walimu na baadaye kuyafuata majibu na kuyasambaza ndani ya chumba cha mtihani,” alisema na kuongeza kuwa katika udanganyifu huo hata askari Mgambo Peter Msigwa alihusika.
Alisema katika Shule ya Kondi Kasandalala, Sikonge, Tabora wanafunzi walikutwa wana mfanano wa majibu ya kukosa usio wa kawaida, jambo ambalo lilionesha kuwa walitumia chanzo kimoja cha majibu.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top