0
Mwanamke  mkazi wa Unga-Limited jijini Arusha , Lightness Kivuyo ameripotiwa kufa wakati akifanyiwa maombi nyumbani kwa mchungaji aliyejulikana kama ‘Nabii Rajabu’ eneo la Kwa-Mrombo pia jijini humo.
.

Kwa mujibu wa dada wa marehemu, Juliana Kivuyo, Lightness alikuwa amesindikizwa nyumbani kwa nabii huyo nyakati za usiku na mumewe aliyemtambulisha kama Shafii Mohammed na kwamba wakati akifanyiwa ibada ya maombi, alianguka na kufariki miguuni mwa ‘Mtume,’ huyo.

“Baadaye shemeji alikuja nyumbani akihema, huku anadai kuwa dada alikuwa kwenye hali mbaya kule kwenye maombi,” alisema Juliana na kuongeza kuwa alitoka mbio kwenda Kwa-Mrombo nyumbani kwa Nabii Rajab na kumkuta dada yake amelazwa kwenye kochi, akiwa bila nguo isipokuwa tu khanga alizofunikwa nazo.

Nabii huyo pia anadaiwa kumnyoa nywele zote pamoja na nyusi za macho wakati akimfanyia ‘huduma,’ hiyo.

Polisi jijini hapa wamethibitisha tukio hilo wakiongeza kuwa tayari watu wawili wamekamatwa kutokana na kifo hicho cha ‘maombi tatanishi.’

Aidha, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Charles Mkumbo ameongeza kuwa atatoa taarifa kamili mara baada ya kikao chake na Mkuu wa Mkoa.

Mganga Mkuu katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, Jacqueline Uriwo amekiri kupokea mwili wa marehemu, lakini akasema, “Kwanza walijaribu kutudanganya kuwa huyo mama alikuwa hai na kwamba aliletwa kwa ajili ya matibabu, lakini tukagundua kuwa walichokileta ni mwili mfu, hivyo tukampeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti!.”

Mkurugenzi wa Huduma ya Mazishi katika hospitali hiyo ya mkoa, Dk Francis Coster alisema mwili ulipelekwa hapo na mume wa marehemu ambaye alisisitiza kuwa mkewe hajafa, bali kazimia tu na kwamba mara nyingi huzimia kwa saa nyingi.

Dk Coster aliongeza kuwa ilibidi na wao wasiweke mwili kwenye jokofu na kuulaza kwenye machela kwa saa sita na ndipo wakaamua kuuweka kwenye droo za maiti, kwani ilikuwa wazi sasa kwamba asingeamka tena asilani.

Waganga hospitalini hapo wamekiri kuwa mwili wa marehemu uliletwa hospitalini hapo ukiwa umenyolewa upara, lakini ukiwa na mikwaruzo pamoja na uvimbe hususan maeneo ya mikono na kifua.

Baba mkubwa wa marehemu, Ally Kivuyo ambaye ndiye mlezi wa Lightness, alisema mume wa marehemu alimtaarifu juu ya kifo hicho na kuongeza; “Lakini baadaye nikaletewa taarifa nyingine kuwa Lightness kumbe alikufa wakati akifanyiwa maombi au vitu vingine, nyumbani kwa mtu anayeitwa ‘Nabii Rajabu,’ hapo basi ikabidi niwataarifu polisi ambao walikuja kumkamata mumewe pamoja na huyo anayejiita nabii au mtabiri.”

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top