0
Geita. Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lililopo katika Kijiji cha Bukondo, Peter Msopela amefukuzwa kazi hiyo baada ya kukiri kuwapa mimba waumini wake wawili katika kipindi cha mwaka mmoja.

Akizungumza na mwandishi wetu baada ya kikao cha ngazi za juu za kanisa hilo kilichofanyika juzi, Askofu mkuu wa kanisa hilo, Herryabwana Majebele alisema amemsimamisha kazi mchungaji huyo kwa kuwa amechafua kanisa la bwana.

Mchungaji Msopela amekiri kufanya kosa hilo na amejitetea kwamba alipitiwa na shetani, hivyo kuwataka waumini wamsamehe. Pia amemsihi Askofu Majebele asimfukuze kanisani.

Hata hivyo, Askofu Majebele alisema mchungaji huyo licha ya kulitumikia kanisa kwa kipindi cha miaka sita, kitendo alichokifanya ni kuvunja Amri 10 za Mungu.

“Kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kwa waumini wakimtuhumu Msopela kuwabebesha mimba wanawake wawili wa kanisa lake na kuwaahidi kuwaoa. Ushahidi upo kutoka kwa waliotendewa vitendo hivyo, nimemfukuza kazi ya uchungaji ili akaendelee na starehe zake huko kwingine,” alisema Majebele.

Baada ya kumvua wadhifa huo, Askofu Majebele alisema kanisa hilo sasa litakuwa chini ya uangalizi wa Mwinjilisti Malisafi Damasi hadi pale atakapoletwa mchungaji mwingine.

Mmoja wa waumini waliopewa mimba na mchungaji huyo, Sarah Muhayiwa alisema alianza uhusiano wa kimapenzi naye tangu mwaka jana na kwamba baada ya kubeba ujauzito, alianza kumshauri asiseme jambo hilo kanisani akiahidi atamuoa.

“Baada ya hapo alinipangishia chumba mjini Katoro tangu Januari 3 lakini akanitelekeza, muda mfupi nikasikia ametangaza kumchumbia mwanamke mwingine ambaye naye alikuwa na ujauzito wake,” alisema Sarah.

Mzee wa kanisa hilo, Penina Thomas alisema mchungaji huyo amekuwa akifumaniwa mara kwa mara na hivyo anapaswa kuondolewa kwenye nafasi hiyo.

Mwinjilisti Damasi alisema kutokana na tabia hizo, waumini wengi wamekata tamaa ya kuendelea kuhudhuria ibada.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top