0

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemzuia shahidi wa kwanza katika kesi inayomkabili Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na wenzake watatu, kujibu swali linalohusu mamlaka ya kikatiba ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC),  kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25,2015. Kwa mujibu wa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba , swali hilo la Lissu halina mashiko.

Lissu alimuuliza shahidi ambaye ni Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Ilala, Salum Hamduni kwamba, Jecha Salim Jecha ana mamlaka gani kikatiba kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015.

Lissu alimuuliza Kamanda Hamduni kama anafahamu mamlaka yapi ya kikatiba ambayo Mwenyekiti wa ZEC, Jecha aliyatumia kufuta uchaguzi mkuu wa madiwani, wabunge na Rais.

Wakili wa Serikali, Paul Kadushi amedai kuwa shahidi huyo amekwenda mahakamani kutoa ushahidi kuhusu maelezo na kwamba si kutoa tafsiri ya kisheria kuhusu Katiba ya Zanzibar.

Kadushi amedai anapinga shahidi wake kujibu swali hilo kwamba Mwenyekiti wa ZEC ana mamlaka ya kufuta uchaguzi ama la na kueleza kuwa shahidi huyo hana ufahamu wa sheria na si mtaalamu wa Katiba na sheria.

''Napinga shahidi kujibu swali hili ambalo kimsingi linamtaka atafsiri sheria, jambo ambalo silo lililomleta na wala hana utaalamu wa kisheria. Hata hivyo, mahakama hii haina mamlaka ya kutafsiri Katiba isipokuwa ni mahakama ya kikatiba na mahakama kuu ndio yenye uwezo huo,'' alidai Kadushi.

Lissu alipinga hoja hizo kwa maelezo kwamba, pingamizi la wakili wa serikali halina maana kwa sababu suala la mamlaka halali au si halali ya Zanzibar limeletwa na upande wa mashitaka wenyewe, kama ambavyo mashitaka ya pili katika kesi hiyo wameeleza kuwa habari iliyochapishwa ingeweze kuleta chuki kwa Wazanzibar kuichukia nchi yao.

Alidai kuwa, masuala ya mamlaka wameyaleta wenyewe wanapaswa kukabiliana nayo, kwa kuwa Sheria ya Ushahidi namba 147, kifungu kidogo cha pili na Sheria namba 157 ya sheria hiyo, vinaweka wazi kwamba shahidi anaweza kuulizwa swali lolote na kwamba si lazima liwe ndani ya kile anachokitolea ushahidi.

Hakimu Simba amesema, mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuzungumzia Katiba ya Zanzibar.

Amesema mahakama katika kesi hiyo haitazungumzia uhalali au kutokuwa halali kwa Mwenyekiti wa ZEC, Salim Jecha kufuta au kutofuta uchaguzi mkuu Zanzibar.

"Pingamizi la upande wa mashitaka ambao ulipinga masuala ya kikatiba ambayo mbunge huyo alikuwa akimuuliza shahidi kuhusu Jecha ana mamlaka gani kikatiba kufuta uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, 2015, ni sahihi na shahidi hatakiwi kujibu swali hilo," amesema Hakimu Simba.

Lissu amedai uamuzi huo hautamuathiri na kwamba anakubaliana nao kwamba haruhusiwi kuuliza swali hilo kwa shahidi hivyo waendelee na ushahidi.

Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 8 na 9, mwaka huu na kuutaka upande wa mashitaka kupeleka mashahidi ili kesi iishe kwa kuwa watu wengi wanaifuatilia hivyo iishe waendelee na shughuli za maendeleo.

Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Mhariri wa gazeti la Mawio, Simon Mkina, mwandishi wa gazeti hilo, Jabir Idrisa na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.

Wanadaiwa kati ya Januari 12 na 14, mwaka huu, Dar es Salaam, kwa lengo la kuleta chuki kwa wananchi wa Zanzibar, Jabir, Mkina na Lissu, kwa pamoja waliandika na kuchapisha taarifa‎ za uchochezi zenye kichwa cha habari kisemacho, 'Machafuko yaja Zanzibar'.

Katika mashitaka yanayomkabili Mehboob, anadaiwa kuwa, Januari 13 katika jengo la Jamana, Dar es Salaam, alichapisha gazeti la Mawio lililokuwa na taarifa za uchochezi, pia alichapisha gazeti hilo bila ya kuwasilisha hati ya kiapo kwa Msajili wa Magazeti.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top