Dodoma, Alhamisi, 2 Februari, 2017:
Serikali imetoa ufafanzi kuhusu masuala mbalimbali kuhusu utawala wa
Sheria na kuainisha mikakati yake katika kuzuia au kupunguza athari za
matetemeko ya ardhi nchini. Ufafanuzi huo umetolewa mjini hapa leo.
Serikali Kutoingilia Mihimili ya Dola
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesisitiza kuwa Serikali inaheshimu mgawanyo wa
mihimili mitatu ya dola nchini. Waziri Mkuu alikuwa akifafanua kuhusu
malalamiko kuwa baadhi ya wafuasi wa vyama vya siasa kesi zao zinachukua
muda mrefu.
Aidha,
Waziri Mkuu amekanusha vikali madai kuwa Serikali inakusudia au
imetangaza kufuta vyama vya siasa hasa vya upinzani nchini madai
yaliyotolewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Bw. Freeman Mbowe.
Mkakati Kuzuia Majanga Ya Asili
Akijibu
hoja kuhusu mikakati ya kupambana na athari za majanga ya asili, Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Ajira), Anthony Mavunde,
amesema Serikali tayari inao mkakati wa kitaifa wa kupambana na majanga
ya asili yakiwemo matetemeko.
Aidha,
Serikali imeandaa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo
imeainisha aina mbalimbali za maafa ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na
majukumu ya kila mdau katika kushughulikia maafa. Aliongeza kuwa,
Serikali pia imeandaa Mwongozo wa Taifa wa Kukabiliana na Maafa ambao
unaelekeza Taasisi kiongozi na wajibu wao wakati wa kukabiliana na
majanga.
Liganga, Mchuchuma Kuzalisha Megawati 350
Serikali
imesema kuwa, miradi unganishi ya Mchuchuma na Liganga itakayotekelezwa
kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) na Kampuni ya Sichuan
Hongda Group (SHG) Limited ya China kupitia ubia wa pamoja wa Tanzania
China International Mineral Resources Limited (TCIMRL) itazalisha zaidi
ya ajira 33,000 na kuipatia nchi umeme wa megawati 350.
Akitoa
ufafanuzi huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani
amesema kuwa kampuni hiyo imeshapewa leseni na vibali vingine muhimu na
sasa inakamilisha ulipaji wa fidia ili kuanza kazi. “Miradi hiyo
unganishi itawezesha kuchimbwa makaa ya mawe kiasi cha tani milioni (3)
na chuma ghafi tani milioni 2.9 kwa mwaka,” alisema.
Usalama wa Raia Mipakani
Serikali
kupitia vyombo vya ulinzi na usalama katika maeneo ya mipaka inachukua
hatua za pamoja na vyombo vya nchi jirani kuhakikisha usalama wa
wananchi na mali zao katika maeneo hayo.
Akijibu
hoja kuhusu suala la usalama wa raia wanaoishi pembezoni mwa mipaka ya
Tanzania, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni, amefafanua kuwa operesheni za pamoja zinafanyika katika mipaka
ya nchi na vikao vya ujirani mwema ili kuhakikisha usalama. Wananchi
wameombwa kutoa taarifa wanapowaona wageni wasioeleweka katika maeneo
yao ili kuimarisha usalama.
Wanahabari Waendeleze Kiswahili
Serikali
imewapa changamoto wanahabari nchini kuwa chachu ya kuendeleza lugha ya
Kiswahili. Wakijibu maswali mbalimbali ya wabunge kuhusu matumizi ya
Kiswahili fasaha katika vyombo vya habari, Waziri na Naibu Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, wameliambia Bunge kuwa, ni vyema
sasa hata wamiliki wa vyombo vya habari wakaanza kuzingatia ufaulu kwa
somo la Kiswahili kabla ya kuwaajiri waandishi.
Kwa
upande wake Waziri Nape akitoa majibu ya nyongeza, alisema kuenziwa kwa
Kiswahili nchini kumeipa Tanzania hadhi ya kuwa makao makuu ya taasisi
mbalimbali za Afrika zinazojihusisha na maendeleo ya lugha ya Kiswahili.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
Post a Comment
karibu kwa maoni