Wanasheria
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), wamesema wamemshauri
Mwenyekiti wao wa Taifa, Freeman Mbowe, asiende kuripoti polisi leo.
Mwanasheria
wa Chadema, John Mallya, amesema Mbowe hatakwenda kuripoti polisi leo
kwa sababu amefungua kesi ya kikatiba Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es
Salaam na inaanza kusikilizwa Februari 21 mwaka huu.
“Mbowe haendi polisi, tumemshauri asiende kwa sababu kesi yake inaanza kusikilizwa Jumanne (kesho).
“Kama wanamhitaji, waje keshokutwa (kesho) Mahakama Kuu, watampata hapo,”alisema Mallya.
Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu, alisema yuko Mwanza na hajawasiliana na Mbowe.
“Hapa niko Mwanza sijawasiliana na mwenyekiti, lakini kama nikiwasiliana naye, nitamshauri asiende huko polisi.
“Kwa
hiyo, naweza kusema kilichofanywa na Kamishna Sirro si wito wa kipolisi
bali ni siasa kama ambavyo alifanya Makonda kwa kutangaza majina ya
watu hadharani.
“Wito wa polisi huwa ni wa kimaandishi, hawajamwandikia barua, hawajampigia simu.
“Hawa
maafande wana namba zetu za simu sisi kama mawakili wa chama, kama
wanamhitaji Mbowe kwanini wasitupigie simu mpaka watangaze kwenye vyombo
vya habari,”alihoji Lissu.
Alipoulizwa
kama Mbowe atakamatwa wakati wowote kuanzia sasa, Lissu alisema
watalazimika kulishtaki mahakamani Jeshi la Polisi kwa kitendo hicho.
“Hatuwezi kukubali utaratibu huu, waache kufanya siasa, wakimhitaji mwenyekiti wetu wamwandikie barua,”alisema Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki.
Mwanzoni
mwa mwezi huu, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja
majina 65 ya watu wanaodaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya
akiwamo Mbowe.
Pamoja
na kutaja majina hayo, Makonda aliwaagiza watuhumiwa hao kuripoti Kituo
Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa dhidi ya tuhuma
hizo.
Februari
10 mwaka huu, akiwa mjini Dodoma, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai,
alizungumza na waandishi wa habari na kusema hajawahi kujihusisha kwa
namna yoyote na biashara ya dawa za kulevya na pia hatakwenda polisi
kuhojiwa kama alivyoagizwa na Makonda.
Hata hivyo, alisema atakwenda polisi, kama jeshi hilo litafuata taratibu za kumuita kwa mujibu wa sheria.
“Siwezi
kwenda polisi kwa wito wa Makonda kwa sababu hana mamlaka hiyo
kisheria. Kama polisi wananihitaji, waniite kwa kufuata utaratibu,
nitakwenda kwa sababu mimi siogopi kwenda polisi,”alisema Mbowe.
Wakati
Mbowe akisema hayo, juzi Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Simon Sirro, alisema Jeshi la Polisi linamtafuta Mbowe na kwamba
limeshindwa kumpata kwa sababu amezima simu.
Kutokana
na hali hiyo, Kamanda Sirro alitoa saa 48 kwa Mbowe kuripoti polisi na
endapo hatafanya hivyo atatafutwa kwa namna ambayo jeshi hilo litaona
inafaa.
“Jumatatu (leo) asiporipoti kutakuwa hakuna namna ya kulizuia tena Jeshi la Polisi kutafuta namna ya kumhoji.
“Mbaya
zaidi juzi tumejitahidi kumtafuta hapatikani, tulikwenda nyumbani kwake
hakupatikana, tulikwenda mahali anakoishi sasa, pia hakupatikana,”alisema Sirro
Post a Comment
karibu kwa maoni