Benny Mwaipaja,
WFM, Zanzibar
MAMIA ya wastaafu
wa Taasisi za Muungano kutoka visiwa vya Pemba na Unguja-Zanzibar, wanaolipwa na
Wizara ya Fedha na Mipango ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wamejitokeza kwa
wingi kuhakikiwa huku wakiiomba Serikali iwaongezee pensheni kutokana na wengi
wao kukabiliwa na hali ngumu ya maisha.
Wakizunguza katika
Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, iliyoko katika eneo la Vuga,
wastaafu hao wamepongeza hatua ya Serikali ya kuwahakiki ili kufahamu hali zao na
kwamba hatua hiyo itasaidia kuwabaini watu wasio na sifa ya kupata malipo hayo kutoka Serikalini
Wastaafu Bi Sauda
Ramadhani Mpambalyoto na Abuu Ali Hamisi, wameiomba Serikali iangalie namna ya
kuwaongezea pensheni wataafu ambao wengi wao ni wagonjwa hawajiwezi na wengine
wana afya njema, wanalima, lakini wanahitaji kuwezeshwa na Serikali ili waweze
kumudu maisha ambayo wamesema yamepanda.
Mkaguzi wa Ndani
Mkuu wa Serikali Msaidizi, Bw. Stanslaus Mpembe, amesema kuwa Wizara ya Fedha
na Mipango inaendesha zoezi la kuhakiki wastaafu wanaolipwa pensheni na wizara
hiyo ili kuhuisha taarifa za wastaafu kwa lengo la kupata kanzidata (database) iliyo
ili kuiwezesha Serikali kuwalipa wastaafu wanaostahili.
Amesema kuwa wastaafu
wanaolipwa na Wizara hiyo ambao hawatahakikiwa wataondolewa kwenye orodha ya
malipo ya pensheni kwa kuwa watakuwa wamekosa sifa.
Aidha Bw. Mpembe
amesisitiza wastaafu hao kufika wenyewe na sio kutuma wawakilishi, wakiwa na
nyaraka zote muhimu zikiwemo barua ya tuzo la kustaafu, barua ya kustaafu au
kupunguzwa kazini, nakala ya hati ya malipo ya kiinua mgongo au mkupuo, barua
ya ajira ya kwanza, kitambulisho cha pensheni, barua ya kuthibitishwa kazini, kadi
ya benki na picha mbili ndogo zilizopigwa hivi karibuni.
Amesema kuwa zoezi
la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa na Hazina, litakamilika Mkoa wa Dar es salaam
kuanzia Machi 6 hadi 10, mwaka huu 2017
Zoezi hilo la
uhakiki linaloendelea Zanzibar, lilianza Oktoba 20, 2016 katika mkoa wa Pwani
na limeshafanyika katika mikoa 25 ya Tanzania Bara ambayo ni Mbeya, Iringa, Njombe,
Ruvuma, Songwe, Katavi, Rukwa, Morogoro, Dodoma, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Manyara,
Tanga, Mwanza, Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kigoma na Tabora, Lindi
na Mtwara.
Post a Comment
karibu kwa maoni