Maishani, watu wengi hutaka kuishi katika nyumba nzuri na za kifahari.
Wengi huwa hawafanikiwi. Lakini nchini Mexico, ambapo ulanguzi wa
mihadarati umekithiri, wakuu wa magenge ya ulanguzi wa dawa za kulevya
huishi maisha ya kifahari, na huendeleza hizi hata wanapokuwa wafu.
Nchini humo, utapata makaburi ambayo yangegeuzwa kuwa nyumba, matajiri wengi wangejivunia kuishi.
Ni makaburi makubwa yaliyojengwa na kuwekwa huduma za kisasa na vitu vingi vya anasa.
Kuna baadhi ya makaburi yenye viyoyozi vya kudhibiti viwango vya joto na
kuingiza hewa safi, kuna vioo visivyopenya risasi na baadhi yana hata
vyumba ambavyo wageni wanaofika kutoa heshima kwa wafu, wanaweza kuketi
na kupata kila kitu kinachopatikana katika nyumba za kifahari.
Baadhi yanakadiriwa kugharimu hadi £230,000 (Sh633 milioni za Tanzania; Sh29 milioni za Kenya)
Hali hii ni tofauti kabisa kwa maelfu ya watu wanaouawa katika
makabiliano ya magenge ya ulanguzi wa dawa hizo za kulevya ambao sana
huzikwa katika makaburi ya pamoja au miili yao kutungikwa na kuachwa
ikiwa imening'inia kwenye madaraja.
Ni mwongo mmoja sasa tangu serikali ya Mexico ilipotuma wanajeshi wake kwenda kukabiliana na magenge ya walanguzi.
Lakini walanguzi wakuu, ambao wamejipatia pesa nyingi, wanaweza kupamba
makaburi yao kutokana na pesa walizolimbikiza kutokana na biashara hiyo.
Makaburi mengi haya hupatikana jimbo la Sinaloa, anamotoka mlanguzi mkuu
Joaquin "El Chapo" Guzman ambaye kwa sasa anazuiliwa na anatarajiwa
kuhamishiwa Marekani mwakani.
Katika eneo moja la makaburi, Jardines del Humaya, katika mji mkuu wa
jimbo la Culiacan, ndipo unapopata baadhi ya makaburi ya kupendeza
zaidi.
"Ni ishara ya nguvu na mamlaka ambayo wakati mmoja walikuwa nayo na ni
ishara ya matamanio yao ya kutaka kuishi daima, jambo ambalo ni kawaida
kwa binadamu yeyote yule," anasema Juan Carlos Ayala, profesa wa falsafa
katika chuo kikuu cha Autonomous University cha Sinaloa ambacho
huangazia sana utamaduni wa ulanguzi wa dawa.
"Pia ni onesho kwa wale ambao wanaendelea kuishi kwamba mtu huyu alikuwa mtu mashuhuri."
Mwendelezo wa filamu za Netflix, Narcos, umekuwa ukitoa kidokezo kwa
wengi duniani kuhusu maisha yalivyo kwa walanguzi wa mihadarati.
Lakini nchini Mexico, serikali inatafakari uwezekano wa kupiga marufuku
filamu kama hizo, kama njia ya kuwazuia watoto kutazama maisha ya
ulanguzi wa mihadarati kama ya kuvutia.
"Ulanguzi wa mihadarati unakolea katika jamii, kupitia utamaduni, na
sasa tuna tatizo la kutazama umeanzisha wapi na umefikia mwisho wapi,"
alisema Ayala.
Kaburi moja ambalo linadaiwa kuwa na mwili wa mlanguzi aliyetumiwa kuua
watu, lina hata kamera za kiusalama, pamoja na kioo kisichopenya risasi.
Lina pia kuba lenye taa ambazo huwaka. Ndani kuna visu vinne vilivyofungiwa kwenye kijisanduku kilichoundwa kwa vioo.
Baadhi ya makaburi yamejengwa kama nyumba za kisasa au makanisa madogo.
Krismasi inakaribia, na baadhi hata yamewekewa miti bandia ya Krismasi.
Lakini kinachokosekana katika makaburi mengi ni utambulisho wa aliyezikwa ndani.
Santa Muerta, mtakatifu wa kifo, ambaye hatambuliwi na Kanisa Katoliki
la Kirumi, hutukuzwa sana na mamilioni ya watu Mexico, wakiwemo
wahalifu.
"Kuna mchango mkubwa wa dini katika utamaduni wa ulanguzi wa dawa, kwa
sababu iwapo kuna mtu anayehitaji sana ulinzi kutoka kwa miungu au
Mungu, basi ni mlanguzi wa mihadarati ambaye anaweza kuuawa kwa kupigwa
risasi na magenge hasimu au maafisa wa serikali wakati wowote," anasema
Andrew Chesnut, mwandishi wa kitabu kwa jina Devoted to Death: Santa
Muerte, the Skeleton Saint (Kujitolea kwa Kifo: Santa Muerte, Mtakatifu
wa Kiunzi cha Mifupa).
Post a Comment
karibu kwa maoni