0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amelifuta agizo lililotolewa jana tarehe 16 Machi, 2017 na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe linalotoa sharti la kuwa na cheti cha kuzaliwa kwa watu wote watakaofunga ndoa kuanzia tarehe 01 Mei, 2017.

Rais Magufuli amefuta agizo hilo leo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari muda mfupi kabla ya kuondoka katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kurejea Jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli amesema Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji.

Amesema mpaka sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.

“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe” Amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ametoa wito kwa wanasheria kuziangalia vizuri sheria zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete mkanganyiko kwa wananchi. 

Hata hivyo Mhe. Rais Magufuli ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kupata vyeti vyao vya kuzaliwa kama kawaida na amewataka viongozi wote kuwahamasisha wananchi kuwa na vyeti hivyo.
Baada ya tamko kutoka kwa waziri Mwakyembe watu wengi walihoji kwanini kaamua kuchukua uamuzi huo huku Mbunge wa jimbo la Monduli Julius Kalanga akiandika katika ukurasa wake wa Facebook....https://www.facebook.com/jkalanga1 "NIMEPITIA SHERIA YA NDOA SIJAONA MAHALI PANAHITAJIKA CHETI CHA KUZALIWA KM KIGEZO CHA KUFUNGA NDOA.
MM NAJUA KIGEZO NI UPENDO TU'.
"Tumpuuze huyu bwana tuendelee.na mengine".

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top