0
Jeshi la Polisi mkoani hapa limefanikiwa kupata jumla ya bunduki kumi za aina nne tofauti zikiwemo Sub-Machine Gun sita baada ya operesheni ya wiki mbili iliyoanza tarehe 15.02.2017 katika wilaya ya Ngorongoro.

Akitoa taarifa hiyo kwa waandishi wa habari leo asubuhi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo alisema silaha hizo zilipatikana katika vijiji vya Olorieni Magaiduru, Oldonyosambu na Sale vilivyopo katika tarafa za Loliondo na Sale.

Alisema mafanikio hayo yalitokana na taarifa fiche ambazo zilibainisha kwamba kuna baadhi ya watu wanamiliki silaha za kivita hivyo mahojiano makali baina ya askari wa Jeshi la Polisi na Viongozi wa Kimila na kuwataka wasalimishe silaha popote pale ambapo walikuwa wanaamini kwamba silaha hizo zitawafikia Jeshi la Polisi.

Akibainisha vijiji ambavyo silaha hizo zilipatikana kuwa ni Olorieni Magaiduru zilipatikana silaha aina ya Chinese 56 SMG moja yenye namba MT. 70B 1 2730021 na risasi 21 pamoja na silaha aina ya Semi Automatic Rifle (S.A.R) yenye namba KN 250374 ikiwa na risasi nne.

Katika kijiji cha Oldonyasambu ilipatikana silaha aina ya Mark IV yenye namba ZKK 5602 pamoja na silaha nne aina ya Chinese 56 Sub-Machine Gun (SMG) zikiwa na risasi 19. Silaha hizo nne ni Chinese 56 SMG yenye namba RT 7663, bunduki ya pili namba yake ni 563631144 na bunduki mbili nyingine hazikuwa na namba.

Kamanda Mkumbo alisema katika kijiji cha Sale silaha aina ya Chinese 56 SMG yenye namba 89020539 ikiwa na risasi 15 kwenye magazine ilipatikana pamoja na silaha nyingine mbili tofauti ambazo ni S.A.R yenye namba 25032534 na Mark III yenye namba 263126.

Aidha kamanda Mkumbo aliwataka wananchi wanaomiliki silaha za moto kinyume cha sheria wazisalimishe mara moja kwenye ofisi za mitaa, vijiji na hata vituo vya Polisi vyovyote vilichopo karibu huku akitoa onyo kwa wale ambao watakaidi na wakikutwa nazo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao. 

Alisema Operesheni hiyo ni endelevu na itakuwa katika maeneo tofauti ya mkoa huu na si wilaya ya Ngorongoro pekee.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top