Watu tisa (9) wamejeruhiwa katika vurugu wakati wa kuwaondoa wafanyabiashara wadogowadogo sehemu zisizo ruhusiwa wilayani Nyamagana, mkoani Mwanza
Taarifa ya Kamanda wa Polisi Mkoa w Mwanza DCP Ahmed Msangi imesema kwamba tukio hilo limetokea mnamo tarehe 05.03.2017 majira ya saa15:45hrs katika mtaa wa Buhongwa Center ambapo watu tisa wakiwemo askari mgambo wa jiji la mwanza saba (07), afisa mazingira mmoja (01) na dereva wa jiji mmoja (01) walijeruhiwa.
Amesema watu hao walijeruhiwa kwa kupigwa na mawe sehemu mbalimbali ya miili yao na wafanyabiashara wadogowadogo waliokuwa wakifanya biashara pembeni ya barabara wakishirikiana na watu wengine waliokua wakishabikia wakati wakiendelea na zoezi la kuwaondoa wafanya biashara wadogowadogo katika maeneo yasiyo ruhusiwa haswa kwenye hifadhi ya barabara ya mwanza kwenda shinyanga.
Aidha, Msangi amesema katika harakati za kudhibiti vurugu hizo askari walifanikiwa kuwakamata watu tisa ambao inadaiwa kuwa walikuwa wakihusika katika vurugu hizo kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi utakapokamilika, watafikishwa mahakamani.
Majeruhi wote wapo hospitali ya mkoa ya Sekou Toure wakiendelea kupatiwa matibabu na hali zao inaendelea vizuri.
Post a Comment
karibu kwa maoni