Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) imekubaliana na Washirika wa
Maendeleo kurejesha uhusiano wa karibu na wenye tija ili kusaidia
kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa
miaka Mitano pamoja na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanziba (MKUZA III).
Hayo
yamebainishwa mjini Dodoma na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango, Bw. Doto James, wakati akifungua mkutano wa Mazungumzo ya
kimkakati kama ilivyobainishwa kwenye Mwongozo wa Ushirikiano wa
Maendeleo kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo.
Bw.
James amesema kuwa Mwongozo huo wa miaka 7, kuanzia mwaka wa fedha
2017/2018 hadi 2014/2025, umelenga kuipa Serikali nafasi ya kuongoza
mchakato wa maendeleo na kuijengea Serikali uwezo wa kukusanya mapato
yake ya ndani, kuchambua fursa muhimu za uwekezaji na kutumia masoko ya
kikanda na kimataifa kupata faida.
"Tumekubaliana
kwamba tutasimamia mchakato mzima wa maendeleo sisi wenyewe kama nchi,
matumizi mazuri ya rasilimali, kuimarisha uwajibikaji, kukuza biashara
na uwekezaji wa ndani na nje" alifafanua Bw. James
Amesema
kuwa nchi inajivunia hatua kubwa iliyofikiwa kiuchumi na kijamii ambayo
Tanzania imefikia, ikiwemo kutambuliwa kimataifa kuwa kinara wa masuala
ya ukuaji wa uchumi wa Taifa na uchumi jumuishi, ambapo imekuwa
ikifanya vizuri kimataifa, kikanda na katika nchi zilizo kusini mwa
Jangwa la Sahara.
Akizungumza
katika mkutano huo uliowashirikisha Washirika wa Maendeleo kutoka nchi
mbalimbali duniani, Mratibu wa Umoja wa Mataifa na kiongozi wa washirika
hao Bw. Alvaro Rodriguez, ameahidi kuwa watashirikiana na Tanzania ili
malengo yake ya maendeleo yaweze kufikiwa kwa kuboresha zaidi
ushirikiano ambao hapo awali ulianza kulegalega.
Ameelezea
kuridhishwa na hatua zinazochukuliwa na Serikali zote mbili-Tanzania
Bara na Tanzania Zanzibar katika kufanikisha malengo yake ya kukuza
uchumi kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo (FYDPII)
na Mkakati wa Kukuza Uchumi Zanzibar (MKUZA III).
Amesema
ili mipango hiyo iweze kufanikiwa kuna umuhimu wa kuishirikisha
kikamilifu Sekta Binafsi pamoja na washirika wa maendeleo kwa kuweka
mazingira ya kuongeza uzalishaji, kukuza ajira kwa vijana wa kike na wa
kiume na hatimaye kufanya mapinduzi ya kiuchumi.
"Vijana
takribani milioni moja wanaingia katika soko la ajira kila mwaka, hivyo
ni muhimu kuweka mazingira ya upatikanaji wa ajira tena zenye staha
katika kipindi hiki ambacho nchi inafanya mapinduzi makubwa ya viwanda
na uchumi" alisisitiza Bw. Rodriguez.
Amesema
kuwa uwekezaji katika masuala ya elimu, afya, hifadhi ya jamii, kutoa
fursa sawa kwa wote (wanaume na wanawake) ni muhimu kwa kuwa jamii yenye
afya itashiriki vizuri katika masuala ya uzalishaji.
Ameahidi
kuwa Wadau wa Maendeleo wako tayari kusaidia jitihada hizo ili
kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia malengo hayo kwa kuwezesha
miundombinu ya ukusanyaji mapato yake ya ndani, usimamizi na matumizi
mazuri ya fedha za umma, kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika
miradi ya kielelezo pamoja na kusaidia kuibua sera bora na kufadhili
miradi yake ya maendeleo.
Serikali
na Washirika wa Maendeleo wamekubalina kukutana mara mbili kwa mwaka
ambapo kikao kingine kinatarajiwa kufanyika mwezi Novemba, 2018.
Post a Comment
karibu kwa maoni