0
KAIMU jaji mkuu wa mahakama ya Tanzania  Profesa  Ibrahimu  Juma  amesema  takwimu zinaonyesha  mahakama za mwanzo nchini kufanya vizuri katika kusikiliza mashauri yanayofunguliwa na kuyafanyia  uamuzi  kwa  kiwango  cha juu ukilinganisha na mahakama zingine.

Hayo  yalithibitishwa jana na jaji huyo mjini hapa wakati  akizungumza na  mahakimu pamoja na watumishi wa mahakama wa mkoa wa Manyara ikiwa ni ziara yake ya kwanza kuanza kuzungukia mikoa ili kuangalia utendaji kazi  wa watumishi wa mahakama na changamoto zao.

Mapema alipoanza kuzungumza na  mahakimu hao na watumishi alisema mahakama za mwanzo  zimeonekana kufanya vizuri katika mashauri  yanayofunguliwa na kusikilizwa na kutolewa uamuzi  kwa asilimia 71 nchini kote.

“ Kazi tunayoifanya mahakimu ni kubwa sana  kama kungekuwa kunatolewa nishani  mahakama za mwanzo ndio wangeipata na wala siyo mahakama kuu au mahakama ya rufani,’’Alisema  jaji Juma    
Aidha alisema  kwa mujibu wa takwimu kua mahakama zilizofuatiwa  kwa kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi ni mahakama za wilaya kwa asilimia 14, mahakama za hakimu mkazi asilimia saba, mahakama  kuu asilimia tano na mahakama ya rufani asilimia 0.5.

Alifafanua kua  kufanya vizuri  kwa mahakama hizo siyo kwamba ni mahakimu wanaohukumu ndio wamesababisha bali ni utendaji  mzuri unaoanzia kwa watumishi wengine wa mahakama hizo.

“Lugha tunayoitoa kwa wananchi  na mawakili  inaweza kupunguza imani na mahakama  hivyo sisi tuna jukumu kubwa sana la kuhakikisha imani yetu kwa wananchi isipungue au kupotea,’’Alisisitiza
Alitumia fursa hiyo kuwaasa kua wazitumie nguzo tatu  ili kuimarisha utoaji huduma kwa wananchi ambazo ni utawala bora,upatikanaji wa haki na kuimarisha imani kwa wananchi na ushirikishwaji wa wadau.

Alisema iwapo ikitokea mtumishi mmoja au hakimu yeyote akakiuka maadili  atasababisha muhimili mzima  wa mahakama unapakwa matope  kuwafanya wananchi wasiuhamini tena wakati wananchi wao ndio wanastaili kuhudumiwa vizuri kwa kua ndio wafalme wa watumishi.

Naye Hakimu mkazi na mfawidhi wa mahakama ya mkoa  Devotha  Kamuzola  alisema changamoto wanazokabiliana nazo ni uchakavu wa majengo ambapo uchakavu huo ulipelekea mahakama tisa kufungwa.

Hakimu huyo aliungana na kaimu jaji mkuu kua mahakama za mwanzo zinafanya vizuri ambapo katika mkoa huu  mahakama za mwanzo haziishi na kesi  zenye umri wa miezi  mitatu na kwa sasa unakuta kuna zingine zinakua na kesi ambazo hazifiki miezi hata mitatu.

Kamuzola anasema kuwa anajivunia katika mkoa wake  mahakama za mwanzo  zimefanya vizuri mpaka kufikia hatua  mahakama zingine hazina kesi za kusikiliza akitolea mfano wa mahakama ya Dareda iliyopo wilaya ya Babati.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top