0
IDARA ya Maliasili na Utalii wilayani  Babati, mkoani Manyara imeiingizia Serikali mapato ya zaidi ya shilingi milioni 23 zilizotokana na makosa na adhabu mbalimbali zilizotozwa kufuatia uharibifu wa misitu.

 Akizungumza katika kituo cha ukaguzi wa mazao ya misitu kilichopo Sinai mjini Babati, Meneja wakala wa misitu Tanzania wilayani hapa Hamisi Gyori alisema fedha hizo zimetozwa kuanzia kipindi cha July 2016 hadi May 2017 kupitia misitu mine (4) anayoisimamia ndani ya wilaya.

 Gyori alieleza kwamba wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 22 ambapo alifafanua kuwa Zaidi ya shilingi milioni 16 zimetokana na mauzo ya mazao ya misitu wakati Zaidi ya shilingi milioni 7 zimetokana na adhabu kwa watuhumiwa wa uharibifu huo.

 “Wahanga wa adhabu asilimia kubwa ni wale wanaosafirisha mazao ya misitu kama vile mkaa, mbao, na miti kinyume cha sheria na fedha zote hizi zinaingia kwenye Akaunti ya Wilaya ya Babati”, alisema.

 Aidha alibainisha kwamba pamoja na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa karibu kila wiki bado wana changamoto nyingi katika utendaji wao wa kazi ikiwa ni pamoja na ushiriano mdogo wa viongozi wa Serikali za vijiji.

 Aliitaja changamoto nyingine kuwa ni ukosefu wa watumishi na vitendea kazi kama magari, na uharibifu wa mipaka ya misitu ya hifadhi ambapo wafugaji  hufanya shughuli za uchungaji katika maeneo hayo.

“Katika wilaya ya Babati tuna misitu minne (4) ambayo tunaisimamia ambayo ni misitu ya Ufyome, Nnou, Haraa na Bereko yenye jumla ya hekta 25133, ambayo hata hivyo haina usimamizi mzuri kutokana na uhaba wa watendaji”, alifafanua.

 Hata hivyo Gyori aliiomba Serikali kuendelea kutafuta njia ya kuwawezesha wananchi kutumia nishati  mbadala ikiwa ni kupunguza mitungi ya gesi na gesi ili kuepuka wananchi kuzidi kuharibu mazingira kwa kukata miti na kuchoma mkaa kiholela bila utaratibu.

“Sisi ni Wizara ya Maliasili na Utalii lakini tunawawafundisha wananchi jinsi ya kutumia njia nishati mbadala kama vile kujenga majiko banifu ambayo hayatumii kiasi kikubwa cha mkaa na kuni, lakini tuwaombe wenzetu wa Wizara husika ya Nishati na Madini kuwawezesha wananchi hao” alisema Gyori.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top