Mahakama ya Hakimu mkazi wilayani Babati mkoani Manyara, juzi ilimhukumu mkazi moja wa kijiji cha Ndedo Wilayani Kiteto aitwaye Pelo Munga kwenda jela miaka 20 au kulipa faini ya Tsh.29,925,000/- kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa mnamo tarehe 9 Oktoba 2014 Pelo Munga (40) alionekana akitafuta mnunuzi wa meno ya ndovu, na ndipo alipowekewa mtego na shahidi namba mbili katika shtaka hilo ambaye alikuwa ndiyo shahidi wa kuona.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Babati Bi. B. Maziku aliiambia mahakama kuwa mnamo tarehe 9 oktoba 2014 mshtakiwa Pelo Munga akiwa na wenzake watatu huko katika Kijiji cha Ndedo wilayani Kiteto alikutwa na meno 8 ya ndovu yenye uzito wa kilo 32.6 na thamani yaTsh. 29,250,700/- Kinyume cha sheria.
Hakimu Maziku alisema baada ya kusikiliza ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na pande zote mbili, mahakama hiyo iliridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka pasipo kutia shaka kuwa mshtakiwa wa kwanza ndiye aliyekutwa na meno hayo.
Hata hivyo mahakama hiyo ilifikia uamuzi wa kutoa adhabu ya kifungo cha miaka 20 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo ili pia kuwakinga wanyama pori dhidi ya ujangili
Aidha mahakama pia imeamuru vitu vyote alivyokamatwa navyo mshtakiwa vitaifishwe na kuwa mali ya serikali, ikiwemo meno manane ya tembo, mizani moja pamoja na pikipiki.
Awali kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, mwedesha mashtaka wa (TANAPA) l. Bugaba alimwomba Hakimu wa kesi hiyo atoe adhabu kali kwa watu wanaoangamiza wanyama pori ambao ni kitega uchumi cha taifa la Tanzania.
Bw. Bugaba aliendelea kusema kuwa, kutokana na wawindaji hao haramu hivi sasa tembo wamepungua hapa nchini kutoka 100,000 hadi kubakia tembo 30,000 na kusababisha watalii kupungua kuja nchini na kusababishia nchi kukosa fedha za kigeni.
Post a Comment
karibu kwa maoni