0
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi
BAJETI ya pili ya Rais John Magufuli imeendelea kugusa maisha ya wananchi wa kawaida wa Tanzania baada ya kutangaza hatua kadhaa zilizojielekeza kuwaondolea mzigo na kuwafanya wawe na maisha bora.
Bunge jana likiwa na karibu theluthi tatu ya wabunge wote, lilimkatisha kwa nderemo na vifijo Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango, wakati akiwasilisha hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2017/18.
Walifikia hatua hiyo baada ya kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na serikali ambazo zimeonekana dhahiri zitawaondolea mzigo wananchi wa Tanzania. Ilifikia hatua Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliuliza kama awahoji wabunge kwamba Dk Mpango asiendelee na hotuba yake kwani bajeti hiyo imekidhi haja kubwa au kwa maneno ya mtaani “imefunika.”
Miongoni mwa mambo mazuri ya bajeti hiyo ni kufuta ada ya kila mwaka ya leseni ya magari; kufuta ada ya ukaguzi wa viwango vya mazao ya biashara; kutoza kodi ya VAT kwa kiwango cha sifuri kwa huduma zinazotolewa kwenye usafirishaji wa bidhaa/mizigo nje ya nchi.
Pia kuwatambua rasmi wafanyabiashara ndogo wasio rasmi kama machinga, mama lishe, wauza mitumba, kutoza ushuru wa forodha kwa kiwango cha asilimia 0 badala ya asilimia 25 kwenye malighafi na vifaa vinavyoagizwa nje kwa ajili ya kuunganisha na kutengeneza vifaa ambavyo ni mahsusi kwa ajili ya matumizi ya walemavu.
Pia kutoa msamaha wa kodi, riba na adhabu zinazoambatana na madeni yote (Tax Amnesty) ya ada ya leseni ya magari, ni eneo jingine lililowafurahisha wabunge ambao waliserebuka wakishangilia.
Katika kuonesha na kukunwa na bajeti hiyo, Spika Ndugai alisema “haijapata kutokea,” mara baada ya Dk Mpango kukamilisha kusoma hotuba yake akitumia saa 2.09. Kwa mujibu wa Dk Mpango, serikali itaendelea kufanya uchambuzi na tathmini ya tozo na ada zinazotozwa na mashirika, taasisi na wakala mbalimbali ili kuendelea kuweka mazingira bora ya kufanya biashara/kuwekeza na kuondoa kero kwa wananchi.
“Hii itajumuisha kupitia upya na kusawazisha viwango vya tozo na ada hizo na pia kuondoa tozo na ada za usumbufu,” alisema Dk Mpango. Akielezea sura ya bajeti kwa mwaka 2017/18, alisema inaonesha kuwa jumla ya Sh trilioni 31.712.0 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika katika kipindi hicho.
Alisema jumla ya mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 19.977.0, sawa na asilimia 63.0 ya bajeti yote. “Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya shilingi bilioni 17,106.3 sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani.
“Aidha, mapato yasiyo ya kodi ni shilingi bilioni 2,183.4 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni shilingi bilioni 687.3,” alieleza Dk Mpango. Alisema Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.971.1 ambayo ni asilimia 12.5 ya bajeti yote.
Alisema misaada na mikopo inajumuisha miradi ya maendeleo Sh trilioni 2.473.8, mifuko ya pamoja ya kisekta Sh bilioni 556.1 na misaada ya kibajeti (GBS) Sh bilioni 941.2. Alisema serikali katika mwaka 2017/18, itaongeza jitihada za ukusanyaji wa mapato ya ndani pamoja na mikopo ya ndani na nje ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo awamu zinazofuata za ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, na uboreshaji wa bandari mbalimbali nchini, vitatekelezwa kulingana na mpangokaz kutegemea na mwenendo wa mapato ya ndani na nje.
Kuhusu kodi, alisisitiza kuwa kulipa kodi ni wajibu wa msingi wa kila raia kwa maendeleo ya Taifa. “Lazima Watanzania tulipe kodi. Serikali hii haitavumilia uporaji wa rasilimali za nchi na ukwepaji kodi kwa kivuli cha kulinda imani (confidence) ya wafanyabiashara,” alisema Dk Mpango.
Aliwaonya watumishi wa TRA kwamba matumizi ya vitisho na unyanyasaji kwa walipa kodi, kuwadai rushwa na kuwazidishia makadirio ya kodi ili kuwakomoa ni mambo ya hovyo na hayakubaliki hata kidogo.
“Wale watumishi wa TRA ambao naamini ni wachache tu, wanaojihusisha na vitendo hivyo wakome kabisa kufanya hivyo. Wale tutakaowabaini tutawachukulia hatua kali kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma,” alisema.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top