0
Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
RAIS John Magufuli (pichani) amepiga marufuku mpango unaopigiwa debe na asasi ziziso za kiserikali wa kutaka mwanafunzi anayejifungua kurudi shule, kwa maelezo kuwa mpango huo ni laana. Amesisitiza kuwa kamwe katika kipindi cha uongozi wake, hataruhusu jambo hilo.
Akizungumza jana wakati wa kufungua barabara ya Bagamoyo – Msata, Rais Magufuli alisema serikali yake haiko tayari kutoa Sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kusomesha wazazi. Badala yake, alisema serikali inatoa fedha hizo kwa ajili ya wanafunzi wa shule za msingi hadi sekondari wasome bure.
“Tukienda kwa mzaha wa namna hii, tutafika pabaya, mtu amezaa kwa raha zake, mnataka arudi shuleni akiwa na mtoto si atawafundisha wengine! Mnataka akipata mtoto wa kwanza akinyonyesha arudi shuleni, akipata wa pili arudi, akipata wa tatu arudishwe shule, yaani mnataka tusomeshe wazazi?” alihoji Rais Magufuli.
Alisisitiza kuwa hakuna mwenye ujauzito au mtoto, ambaye ataruhusiwa kurudi shuleni katika kipindi cha utawala wake. “Akae nyumbani alee vizuri mtoto wake maana amechagua njia hiyo… tukiruhusu tutawafanya wanafunzi wengine wazae kwa wingi maana mchezo ule ni mtamu na kila mtu atapenda aufanye… chini ya utawala wangu nasema hapana,” alieleza Dk Magufuli kwa sauti ya ukali na msisitizo.
Aliagiza vyombo vya dola kwamba wakati msichana atabaki nyumbani kulea mtoto, wale wanaohusika kuwapa mimba wanafunzi hao, wakafungwe miaka 30 ili nguvu alizotumia kumpa ujazito, akazitumie kuzalisha mali akiwa gerezani.
“Akitoka jela nguvu atakuwa hana tena na yawezekana akakomea mtoto huyo huyo mmoja,” alisema Rais Magufuli ambaye alitoa mwito kwa NGO ambazo zinatetea jambo hilo, zikafungue shule malumu kwa ajili ya wasichana ambao wamejifungua.
Katika suala hilo, Rais alisisitiza kuwa hata kama ni mtoto wake akipata ujauzito akiwa shule, kamwe hawezi kurudi shule. Alizitahadharisha NGO kuwa makini na kunakili mambo ya kigeni kwamba watanakili na mambo ya ajabu yakiwemo ya ushoga, licha ya kuwa wafadhili wa mambo hayo wanakuja na misaada.
“Wakati mwingine tunapata laana za ajabu kwa kufanya mambo yasiyostahili,” alisema Rais Magufuli. Ageukia ufisadi wa pembejeo Rais Magufuli alisema kwa sasa anajiandaa kuchukua hatua kwa mafisadi, ambao walitumia vibaya fedha za pembejeo kwa kuandikisha watu ambao tayari walishakufa ili mradi waibe fedha hizo.
Dk Magufuli alisema anajua miongoni mwa watu waliofanya ufisadi wa fedha za pembejeo, kuna viongozi wa wilaya na mikoa na aliagiza viongozi wa mikoa, kuhakikisha wanawaweka hadharani wale wote ambao walifisadi fedha hizo.
“Mtu anaandikisha maiti, sijui walikuwa wanatoka huko kaburini kuja kuchukua pembejeo, nafanya haya kama kuna sehemu Watanzania tumekosea basi tukatubu dhambi zetu,” alisema Rais Magufuli.
Alimwagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na viongozi wa mikoa na wilaya, kuhakikisha kuwa wanachukua hatua dhidi ya watu wote ambao walishiriki kuiba fedha za pembejeo na kuwaacha wananchi wanyonge wakihangaika.
Ashangaa dawa za malaria Aidha, alisema jana akiwa kwenye kiwanda cha viuatilifu ambavyo ni maalumu kwa ajili ya kuzuia mazalio ya mbu yamejazana kiwandani, lakini watendaji wa Wizara ya Afya wamejikita kwenda kununua dawa za kutibu malaria Ulaya, wanaacha kununua dawa za kuzuia malaria ambayo lita moja inauzwa kwa Sh 13,000 tu.
Alisema iwapo Wizara ya Afya ingetumia dawa hizo, kuangamiza mazalio ya mbu, ndani ya miaka mitano ugonjwa wa malaria ungetokomea. Alisema kuna nchi ambazo zilikuwa na ugonjwa wa malaria kama Uingereza, lakini wameutokomeza kwa kutumia dawa za aina hizo.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli alinunua dawa hizo kwa Sh bilioni 1.3 na amewataka wakurugenzi wote wa wilaya, kuhakikisha wanaenda kuchukua dawa hizo kwa ajili ya kuulia mazalia ya mbu kabla ya Juni 30, mwaka huu. Alisema amefanya hivyo kwa kuwa hataki tena Watanzania wafe kwa ugonjwa wa malaria.
Rais Magufuli alisema kitendo cha wakurugenzi watendaji wa halmashauri, kushindwa kununua dawa hizo, kimemkasirisha na ndio maana wakati mwingine amekuwa anaendelea kutumbua watendaji, ambao hawatimizi wajibu wao.
“Ni wangapi wanataka niendelee kutumbua majipu?” alihoji wananchi ambao walinyoosha mkono, kuonesha kumuunga mkono Rais kwa hatua hizo anazochukua dhidi ya watendaji wabovu.
Awapa wananchi eneo la Magereza Katika hatua nyingine, jana Rais Magufuli alitangaza kuwapa wananchi eneo la Magereza la ekari 65 baada ya wananchi hao, kujitokeza mbele zake wakiwa na mabango, yanayolalamikia unyanyasaji wanaofanyiwa na Magereza ikiwa ni pamoja na kufukuzwa katika eneo hilo.
Baada ya kujitokeza kwa mabango, Rais alitoa ruhusa ya mama mmoja kuzungumza kwa niaba ya wenzake na ndipo mwanamke aliyejitambulisha kwa jina la Asma Msigale kueleza namna ambavyo wamekaa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 50 tangu mababu zao na ndio sehemu wanayotegemea kulipa na kutunza familia zao.
“Sisi tumekaa hapa kwa miaka mingi, lakini sasa tunafukuzwa na Magereza wanasema ni eneo lao, tunakuomba sana Rais utuonee huruma, sisi baadhi ni wajane tunatumia eneo hilo kwa ajili ya kulima na kusomesha watoto wetu, tunaomba watuachie tuendelee kulima,” alisema mwanamke huyo.
Baada ya ombi hilo, ndipo Rais Magufuli alimwita mkuu wa magereza wa mkoa na kumhoji wana eneo la ukubwa wa kiasi gani; akajibu kuwa wana jumla ya ekari 6,186.25. “Mkuu lile eneo lilikuwa na ukubwa wa ekari 75, tumetoa ekari 15 tukawapa halmashauri kwa ajili ya machinjio, zimebaki ekari 65,” alisema mkuu huyo wa magereza.
Kutokana na majibu hayo, Rais aliagiza “Sasa ninyi mna eneo kubwa hata hamlilimi lote, naagiza hizo ekari 65 ni kidogo sana, waachieni hawa wananchi wazimiliki na kuanzia leo zitakuwa za kwao.” Rais pia aligoma kutoa kambi waliyokuwa wanaitumia wakandarasi wa barabara iliyoko Bagamoyo kwa halmashauri.
Alisema hawezi kufanya hivyo kwa kuwa anaamini kwamba magereza inahitaji maeneo makubwa kwa ajili ya wafungwa kulima na kuzalisha mazao mengi. “Tumechoka kuwalisha wafungwa, walime kwa wingi na wazalishe mali… kuna mafisadi ambao watafungwa watalima wapi kama nikianza kugawa maeneo ya Magereza?
Kuna watu wametuibia lazima wafungwe waje kuzalisha mali kwa ajili ya Watanzania,” alisema Rais Magufuli. Gharama za ujenzi Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Patrick Mfugale alisema barabara ya Bagamoyo – Makofia – Msata yenye kilometa 64, imejengwa kwa Sh bilioni 169 na gharama za mkandarasi mshauri ni Sh bilionni nane.
Aliongeza kuwa mkandarasi mjenzi tayari ameshalipwa Sh bilioni 133.7 na mkandarasi mshauri ameshalipwa Sh bilioni 6.9. Mfugale alisema serikali imelipa fidia ya Sh bilioni 4.7 kwa wananchi ambao walistahili kulipwa fidia kwa mujibu wa sheria baada ya nyumba zao kubomolewa na mashamba yao kuchukuliwa.
Mfugale aliongeza kuwa barabara hiyo ambayo imegharimiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Tanzania, mchakato wa ujenzi wake ulianza tangu mwaka 2008, lakini mkandarasi wa awali pamoja na kampuni iliyopewa jukumu la kufanya upembuzi yakinifu, walifukuzwa kutokana na kushindwa kutekeleza kazi kwa mujibu wa mkataba Aliongeza kuwa uwezo wa barabara hiyo ni kudumu kwa miaka 20 iwapo magari yatakayoitumia hayatazidisha uzito.
Uzito wa gari linaloruhusiwa kupita ni tani 56. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema barabara hiyo ni muhimu kwa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa kuwa inapunguza msongamano wa magari yanayotoka Dar es Salaam kwenda sehemu mbalimbali nchini.
Alisema barabara hiyo ni muhimu kwa kuwa inapita maeneo ambako itajengwa bandari mpya ya Bagamoyo. Alisema barabara hiyo, itafungua fursa nyingi za kiuchumi kutoka maeneo ya pwani kwenda maeneo ya kaskazini na maeneo mengine ya nchi.
Profesa Mbarawa alitaja miradi mingine ambayo usanifu umekamilika ni mradi wa njia sita kutoka Dar es Salaam kwenda Chalinze yenye urefu wa kilometa 144, barabara ya Bagamoyo – Sadani hadi Tanga yenye urefu wa kilometa 246. Barabara ya Tegeta – Bagamoyo, barabara ya Makofia – Mlandizi kilometa 36.7 na barabara ya Kibaha hadi Mapinga yeye urefu wa kilometa 24.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top