Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB)
imeahidi kushirikiana na Tanzania kujenga mradi mkubwa wa Reli ya Kati kwa
kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kuipatia mkopo wenye masharti nafuu.
Ahadi hiyo imetolewa Jijini Dar es
Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo anayesimamia kanda ya Afrika
Mashariki, Dkt. Nyamajeje Weggoro, alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji.
Dkt. Weggoro amesema kuwa Benki yake
imeridhika na utendajikazi wa Serikali ya Awamu ya Tano ikiongozwa na Mhe. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli na hivyo kuifanya Bodi ya Wakurugenzi ya Benki hiyo
kukubali kufanikisha ujenzi wa Reli hiyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Amesema kuwa Reli ya Kati kwa Kiwango
cha Kimataifa ni muhimu kwa uchumi wa Taifa lakini pia kwa uchumi wa nchi za
Maziwa Makuu kwa kuunganisha nchi kama vile Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na baadae itaunganishwa na Reli ya Kaskazini
upande wa Kenya.
“Benki iko tayari na inasubiri Tanzania
ilete mapendekezo ama maombi ili yafanyiwekazi, tutakaa pamoja ili tuone Benki
itasaidia kiasi gani na Benki pia inaweza kuwatafuta wadau wengine
tunaosaidiana nao katika miradi mikubwa kama hii” Aliongeza Dkt. Weggoro
Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kati kwa
kiwango cha Kimataifa (Standard gauge), yenye urefu wa kilometa 2,561 umepangwa
kugharimu kiasi cha Dola bilioni 7.6 za Marekani,
sawa na shilingi za Kitanzania Trilioni 16, awamu ya kwanza imeanza kujengwa
kuanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na baadae awamu nyingine zitafuata.
Aidha, Dkt. Weggoro amesema Benki yake
itashirikiana na Serikali kuboresha utendajikazi wa Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) hasa upande wa muundo wake na madeni makubwa yanayolikabili shirika
hilo ili liweze kuchangia ipasavyo ukuaji wa uchumi wa viwanda.
“Benki itatoa fedha ili kulifanya
shirika hilo lifanyekazi kwa ufanisi zaidi, tunajadiliana na tutawashirikisha
pia wadau wengine zaidi ili uamuzi wa Serikali wa kuifanya nchi iwe ya viwanda
uweze kufanikiwa” Alifafanua Dkt. Weggoro
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt.
Ashatu Kujaji, ameishukuru AfDB kwakuwa mshirika mkubwa wa kimkakati wa
maendeleo kwa kusaidia miradi mbalimbali ikiwemo barabara, nishati ya umeme,
kilimo na huduma za jamii.
Dkt. Kijaji amesema kuwa uwekezaji wa
AfDB hapa nchini umefikia Dola bilioni 1.8 huku asilimia 74.5 za uwekezaji huo
iko kwenye sekta ya miundombinu, ambapo barabara imechukua asilimia 51.4,
Nishati (10.1%), Maji na Usafi wa Mazingira (13%) na Sekta nyingine za huduma
za jamii, kilimo na masuala ya fedha (25.5%).
Amesema kuwa uamuzi wa Benki hiyo
kuamua kusaidia ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati kwa kiwango cha
Kimataifa (SGR) pamoja na kuihuisha TANESCO ni hatua muhimu itakayochochea
ukuaji haraka wa uchumi wa nchi.
Ameitaja miradi mingine ya kimkakati
iliyotekelezwa kupitia msaada na mkopo nafuu kutoka Benki hiyo kuwa ni ujenzi
wa barabara ya lami inayoanzia Afrika Kusini-Cairo-Misri-Tanzania, kuanzia
mkoani Iringa, Dodoma hadi Babati mkoani Manyara, inayotarajiwa kukamilika
katika kipindi cha takriban miezi miwili ijayo.
Post a Comment
karibu kwa maoni