0


Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula 
NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula ameliagiza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuzinyang’anya nyumba walizowauzia halmashauri mbalimbali nchini na taasisi za serikali, zilizoshindwa kuzilipia nyumba hizo kwa muda mrefu.
Mabula alitoa kauli hiyo alipofanya ziara kukagua nyumba za NHC zilizojengwa katika eneo la Mlole Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, ambako nyumba 10 hadi sasa hazijalipiwa na Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni licha ya kuzishikilia nyumba hizo kwa zaidi ya miaka mitatu sasa.
Naibu Waziri alisema wanunuzi hasa taasisi za serikali, ambazo ndiyo mlengwa mkubwa wa ununuzi wa nyumba hizo za bei nafuu, kunakwamisha mpango wa shirika wa kuongeza nyumba nyingine katika maeneo mengine nchini.
Alisema jumla ya nyumba milioni tatu za gharama nafuu kwa ajili ya kuishi watumishi wa serikali, zinapaswa kujengwa maeneo mbalimbali nchini, hivyo wanaochukua nyumba hizo hawana budi kuzilipia ili kuwezesha nyumba nyingine kuendelea kujengwa.
Meneja wa NHC Mkoa wa Kigoma, Nistas Mvungi alisema nyumba 10 zilizotolewa kwa Hospitali ya Mkoa ya Maweni, zimeshindwa kulipiwa gharama ya ununuzi zikiwa ni miongoni mwa nyumba 36 zilizojengwa katika eneo hilo.
Mvungi alisema Hospitali ya Maweni ilipewa kipaumbele ya ununuzi wa nyumba hizo wakati Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alipozindua nyumba hizo, lakini hadi leo nyumba hizo zimeshindwa kulipiwa.
Meneja huyo wa NHC alisema hadi sasa asilimia 53 ya manunuzi ya nyumba hizo, imeshalipwa na wanunuzi wengine wanaendelea kulipa kulingana na mikataba yao na NHC

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top