Wizara ya Fedha na Mipango imetiliana
saini na Kampuni ya ujenzi wa barabara ya Reynolds kandarasi ya ujenzi wa
barabara ya kutoka Kidatu hadi Ifakara mkoani Morogoro, yenye urefu wa kilometa
67 kwa kiwango cha lami utakaojengwa kwa shilingi bilioni 101, kupitia ufadhili
wa Umoja wa Ulaya, Marekani na Uingereza.
Mkataba huo umesainiwa na Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban kwa niaba ya Serikali ya
Tanzania na Bw. Dan Yzhak Shahn, Bw. Benjamin Arbit ambaye ni Mkandarasi
kutoka Kampuni ya Ujenzi ya Reynolds.
Kiasi hicho cha fedha
ni sawa na Euro milioni 40.4 ambapo Euro milioni 29.6 zimetolewa
kwa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Misaada la Uingereza-UK-AID,
huku kiasi kinachobaki cha Euro milioni 10.8 kikitolewa na Shirika la
Misaada la watu wa Marekani- USAID.
Akizungumza mara
baada ya kutiwa saini kwa kandarasi hiyo, Bi. Amina Khamis Shaaban, amesema
ujenzi wa barabara hiyo utakaohusisha pia ujenzi wa daraja katika Mto Ruaha
Mkuu, utasaidia wakulima wadogo kupitia Program ya Uendelezaji Kilimo katika
Ukanda wa Kusini mwa Tanzania-SAGCOT, walioko katika Bonde la Mto Kilombero,
kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao.
“Kuimarika kwa kipande hiki cha
barabara kutaongeza uzalishaji wa nafaka na bidhaa nyingine hatimaye kupunguza
gharama za chakula na umasikini wa wananchi” aliongeza Bi. Shaaban
Bi Shaaban amewashukuru wadau hao wa
maendeleo kwa msaada huo utakao fungua milango ya kiuchumi kwa Watanzania
kupitia Program hiyo ya kuendeleza Kilimo katika Ukanda huo wa Kusini-SAGCOT,
unaohusisha pia kuboresha masuala ya nishati ya umeme.
“Ujenzi wa miundombinu unalengo
la kuchochea maendeleo ya kilimo cha kibiashara kwa kuwa itasaidia
kuwakutanisha pamoja wafanyabiashara na wakulima”. Aliongeza Bi Shaaban.
Aidha amesema uboreshwaji wa
miundombinu utachochea uwekezaji ambao ndio chachu ya maendeleo ya biashara za
watu wa chini, hivyo kuinua kiwango cha maisha yao.
“Barabara ya Kidatu hadi Ifakara ndiyo
inayounganisha Wilaya za Kilombero na Ulanga na ni barabara kuu itokayo Bandari
ya Dar es Salaam kwenda Zambia, Malawi na nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Congo (DRC) hivyo kuwa na tija katika kuharakisha maendeleo ya kiuchumi jambo
ambalo ndio lengo kubwa la Wahisani hao”. alifafanua Bi Shaaban.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa
Ulaya (EU) hapa nchini, Roeland van de Geer ameahidi kuwa EU, UKAID na USAID,
zitaendelea kushirikiana kwa kiwango cha juu na Serikali ya Tanzania katika
kuboresha Sekta ya ujenzi na miundombinu kwa ujumla lakini pia atahakikisha
wanachangia katika kupata soko la uhakika la mazao ya kilimo.
Sekta ya kilimo ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania
mbapo zaidi asilimia 70 ya wakazi wake hutegemea kilimo na kuna uwezekano
mkubwa wa kuongeza uzalishaji, kipato na kukuza ajira, hususan kwa wanawake na
vijana ikiwa miundombinu inayochangia ukuaji wa Sekta hiyo itazidi kuimarika.
Post a Comment
karibu kwa maoni