0
Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mjini Iringa kimeanza kumeguka vipandevipande kwa kile kinachoelezwa kina ukandamizi mkubwa wa demokrasia unaofanywa na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Katika tukio la jana madiwani watatu wa Iringa mjini waliochaguliwa kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, wametangaza kujivua uanachama wa chama hicho hatua inayowapotezea sifa ya kuendelea kuwawakilisha wananchi kupitia nafasi hiyo ya kisiasa.
Madiwani hao ni pamoja na Diwani wa Kata ya Kitwiru, Baraka Kimata na madiwani wawili wa Viti Maalumu, Leah Mleleu na Husna Daudi. Wakizungumza na waandishi wa habari mjini Iringa jana madiwani hao wamesema udikteta unaofanywa na Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chadema akiwakilisha mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hauvumiliki.
Akitangaza uamuzi huo, Kimata aliyekuwa pia Katibu Mwenezi wa Jimbo la Iringa Mjini na Mwenyekiti wa Madiwani wa Chadema Mkoa wa Iringa, alisema anatarajiwa pongezi kubwa kutoka kwa wana Chadema wenzao wanaoendelea kuvumilia maumivu wanayopata kutoka kwa kiongozi hiyo.
“Baada ya kupata halmashauri hapa Iringa Manispaa kumekuwa na matatizo makubwa. Kuna tuhuma za rushwa lakini viongozi wakubwa wamekuwa na ubaguzi mkubwa miongoni mwa madiwani,” alisema Kimata.
Alisema Chadema iliwaaminisha Watanzania kwamba ni chama mbadala wa demokrasia ya kweli nchini lakini ukweli hauko hivyo katika jimbo la Iringa mjini. “Nimekuwa na mvutano mkubwa na wa muda mrefu na mbunge wa jimbo la Iringa Mjini na hii imeniweka katika mazingira magumu sana.
Nimevumilia kulinda heshima ya mbunge na chama lakini imefika mwisho lazima niseme siwezi kuvumilia hali hii,” alisema. Alisema amekuwa akihesabiwa kama mmoja wa wasaliti wa chama hicho kwa sababu ya kutofautiana na mbunge huyo na viongozi wengine katika mambo mbalimbali ya uendeshaji wa chama ikiwa ni pamoja na namna alivyopatikana naibu meya mpya katika uchaguzi uliofanyika hivi karibuni.
“Ninaiona hatari mbele yangu kwamba mwisho wa siku naweza kushindwa kufanya kazi kwa viwango vinavyopaswa, hivyo kwa hiari yangu mwenyewe nimeamua kuachia ngazi nafasi zangu zote ndani ya chama na ninaachia nafasi yangu ya udiwani wa kata ya Kitwiru,” alisema.
Alisema anataka viongozi wa Taifa wa chama hicho wafahamu kwamba kuendelea kuwaburuza vijana na wanawake wanaokipenda chama hicho ni kujichimbia kaburi. “Kama kweli Chadema inataka kuchukua dora ipunguze udhalilishaji, unyanyasaji na ukandamizaji unaoendelea ndani ya chama,” alisema.
Naye Leah ambaye ni Katibu wa Baraza la Vijana wa Chadema Iringa Mjini, Ofisa Habari wa Umoja wa Madiwani, Katibu wa Umoja wa Madiwani Iringa Mjini na Diwani wa Viti Maalumu alisema; “Kwa hiari yangu nimeamua kuachia ngazi zote hizo.
Nilifanya kazi kubwa sana wakati wa uchaguzi na nilikuwa mratibu wa uchaguzi wa Jimbo.” Alisema anaipenda demokrasia lakini anaona muelekeo wa chama hicho hauwiani kabisa na demokrasia inayohubiriwa.
“Ndani ya Chadema usipounga mkono mambo binafsi anayotaka Mchungaji Msigwa kwa maslahi yake wewe unageuka adui wa chama. Kiongozi huyo anavuruga chama, haambiliki, anajua kila kitu, hasikii maoni ya wengine na anachoamua yeye ndicho kinachotakiwa kuwa,” alisema na kusema kwa mazingira hayo ameamua kunawa mikono.
Naye Husna ambaye ni mkufunzi wa siasa ngazi ya Jimbo na diwani wa viti maalumu alisema; “leo tarehe 23 nimeamua kujivua uanachama na nafasi zangu zote kama walivyofanya wenzangu kwa sababu ya masimango ninayopata kutoka kwa Mchungaji Msigwa.”

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top