0
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro akionesha magazine za bunduki zilizokamatwa katika operesheni iliyofanywa na jeshi hilo (Picha na Jeshi la Polisi).
POLISI imewaua wahalifu 13 baada ya kutokea kwa majibizano ya risasi na wahalifu hao katika wilaya ya Rufiji mkoani Pwani.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro ameeleza katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba majibizano hayo yalitokea katika Kijiji cha Rungungu wilayani humo, Agosti 9, mwaka huu na majeruhi hao walifariki dunia wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.
IGP Sirro alieleza kuwa kiini cha mauaji hayo ni kukamatwa kwa mtuhumiwa Abdallah Mbindimbi maarufu Abajani, Agosti 4, mwaka huu katika eneo la Gari Bovu, Kijiji cha Chamiwaleni, Kata ya Mchukwi, Tarafa ya Kibiti, Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Kipolisi Rufiji, akiwa ana majeraha maeneo mbalimbali ya mwili wake akionekana kuwa alikuwa anaendelea kujitibia mwenyewe kwa njia za kificho.
“Mtuhumiwa huyu alikamatwa kutokana na kuwepo kwa taarifa za kiintelijensia kuhusu yeye kuhusika na vitendo vya kufadhili, kusaidia, kuhifadhi na kushiriki uhalifu wa ujambazi maeneo mbalimbali. Mtuhumiwa alipohojiwa kuhusiana na tuhuma zinazomkabili alikubali na alionesha dhamira ya kwenda kuonesha ngome yao,” alieleza Sirro.
IGP Sirro aliongeza kuwa Agosti 9, mwaka huu, saa tatu usiku katika mapori ya Kijiji cha Rungungu, mtuhumiwa akiambatana na askari Polisi, alikwenda kuonesha ngome ya watuhumiwa wenzake aliokuwa anashirikiana nao kufanya uhalifu.
“Baada ya kukaribia eneo la tukio ulitokea upinzani mkali wa majibizano ya risasi jambo lililosababisha hata Abdallah Abdallah Mbindimbi kujeruhiwa na risasi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kufuatia majibizano hayo, askari Polisi walifanikiwa kuwajeruhi wahalifu kumi na mbili. Jitihada zilifanyika kuwapeleka hospitali majeruhi wote kumi na tatu ingawa baadaye walifariki dunia kwa nyakati tofauti wakipelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kutokana na kuvuja damu nyingi zilizosababishwa na majereha ya risasi sehemu mbalimbali za miili yao,” alifafanua Mkuu wa Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa IGP Sirro, miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kuwataja watuhumiwa saba kati ya 13, waliopoteza maisha kutokana na majibizano ya risasi, wametambuliwa kuwa ni Hassani Njame, Abdallah Mbindimbi “Abajani”, Saidi Kilindo, Abdulshakuru Ubuguyu, Issa Mseketu “Mtawa”, Rajabu Thomas “Roja,” na Mohamed Kadude “Apolo.”
Aliongeza kuwa miili sita iliyobaki, haikuweza kutambulika mara moja, hivyo utambuzi utaendelea ilikohifadhiwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Aidha, alisema vielelezo mbalimbali vilipatikana katika eneo la tukio, ambavyo ni silaha, risasi na mabomu; na kuzitaja silaha aina ya SMG tano mali ya Jeshi la Polisi zilizoporwa tukio la kupora silaha askari Mtengeni – Jaribu Mpakani; silaha ya kudhibiti vurugu mbili mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora silaha askari Mtengeni – Jaribu Mpakani; SAR moja mali ya Jeshi la Polisi tukio la kupora silaha askari Polisi Stakishari Jijini Dar es Salaam na magazini mbili pia za Polisi zilizoporwa kwa askari Mtengeni – Jaribu Mpakani.
Alitaja silaha nyingine ni risasi za SMG 158 mali ya Polisi zilizoporwa Mtengeni – Jaribu Mpakani, bomu la kurusha kwa mkono moja ambalo uchunguzi dhidi ya bomu hilo unaendelea, mabomu ya kutuliza ghasia manne ya Polisi yaliyoporwa kwa askari Mtengeni – Jaribu Mpakani wilayani Kibiti.
Kuhusu vielelezo vingine, alisema ni pikipiki mbili ambazo zilitumika kuwasafirisha wahalifu hao kwenye utekelezaji wa matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali, vitenge na nguo mbalimbali ambavyo viliporwa baada ya kufanya tukio la kumuua Diwani wa zamani wa Kibwiwi na begi lililoporwa baada ya kumuua Mtendaji wa Kijiji cha Mangwe.
Akieleza zaidi, IGP Sirro alisema kwa mujibu wa taarifa za utambuzi wa vielelezo vilivyopatikana eneo la tukio na utambuzi wa baadhi ya miili ya watuhumiwa waliofariki, inaonesha kuwa walishiriki matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali ikiwamo kuua OC CID na watumishi wawili wa Idara ya Maliasili katika tukio la Jaribu Mpakani – Wilaya Kibiti, kuua askari Polisi wanane katika tukio la Mkengeni – wilayani Kibiti, kuua trafiki wawili katika tukio la Bungu “B” – wilaya ya Kibiti, kumuua Diwani wa zamani CCM katika tukio la Kibwibwi – wilaya ya Kibiti na kuua Ofisa Mtendaji, Mwenyekiti wa Mtaa na mkulima katika tukio la Kijiji cha Mangwi – wilaya ya Kibiti.
IGP Sirro aliwataka wananchi wote nchini, kuondoa hofu ya kwamba eneo hilo la Kibiti si salama, na kuwaomba waendelee kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.
Aidha, aliwaomba wananchi kutoa taarifa mara moja kwa Jeshi la Polisi wanapohisi kuna jambo lolote wanalolitilia mashaka. “Natoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani, hususani maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri, kuendelea na shughuli zao mbalimbali za kujiletea maendeleo.
Nawasihi kwa dhati kabisa waendelee kutupatia taarifa zitakazosaidia kumaliza kabisa uhalifu kwenye eneo hili. Nitumie fursa hii kuwashukuru sana wananchi wa maeneo ya Mkuranga, Kibiti na Ikwiriri kwa ushirikiano mnaotupatia ambao umesaidia sana kuwadhibiti wahalifu.
“Mamlaka za hospitali, zahanati, vituo vya afya, maabara za afya ya binadamu na maduka ya kuuza dawa za kutibu binadamu zijiepushe na utaratibu wa kutoa matibabu kienyeji au kificho kwa watu waliojeruhiwa bila kufuata taratibu za kisheria ikiwemo kupata taarifa ya Polisi “kupitia fomu maalumu ya kuruhusu matibabu (maarufu kama PF. 3)”.
Wahalifu wakijeruhiwa ni lazima watafute matibabu,” alieleza. Aliongeza kuwa wapo baadhi ya watuhumiwa, wafadhili na washirika wa uhalifu na wahalifu wa ujambazi maeneo haya ambao hawajakamatwa.
“Jambo la kufurahisha ni kwamba taarifa zao zipo kwa Jeshi la Polisi nchini na zinaendelea kufanyiwa kazi ili waweze kukamatwa na kufikishwa kwenye mkono wa sheria mara moja,” alibainisha.
Aliwataka wananchi kutoka taarifa kwa Polisi kama inawafahamu watuhumiwa watano ambao wanasakwa ambao ni Anafi Kapelo “Abuu Mariam,” Hassan Kyakalewa “Abuu Salma au Shujaa au Dokta,” Haji Ulatule, Shehe Hassan Mzuzuri na Rashid Mtutula

Polisi Kibiti mkoani Pwani  imethibitisha kuuawa kwa watu kumi na tatu wanaotuhumiwa kufanya vitendo vya uhalifu ikiwemo mauaji ya polisi,viongozi wa serikali za mitaa na vijiji pamoja na wanachama wa chama cha mapinduzi.
Msemaji wa jeshi la polisi Barnabus Mwakalukwa amesema pamoja na mauaji hayo, polisi pia imeweza kukamata baadhi ya silaha ikiwemo bunduki, risasi, mabomu pamoja na pikipiki mbili.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top