Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa
Kanuni za taarifa za Usafirishaji na uingizaji wa fedha taslimu kutoka na
kwenda nje ya nchi (Crossborder Declaration of Currency and Bearer Negotiable
Instruments Regulations) ambapo wasafirishaji wa fedha taslimu na wasafiri wote
wanaotoka au kuingia nchini, watatakiwa kutoa taarifa za fedha taslimu
wanazosafirisha ikiwa fedha hizo zinalingana au zinazidi kiasi cha dola za
kimarekani elfu kumi (USD 10,000).
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa
warsha ya siku mbili ya maandalizi ya utekelezaji wa Kanuni hizo, Kamishna na
Mtendaji Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu (FIU) Ndugu Onesmo H.
Makombe alisema utekelezaji wa kanuni hizi, pamoja na mambo mengine utaiwezesha
nchi kuwa na takwimu za usafirishaji fedha taslimu.
“Takwimu hizo zitakazosaidia pamoja na
mambo mengine kubaini vitendo vya kihalifu, kupunguza utoroshaji wa mitaji na
kuhakikisha kuwa tunapunguza kama siyo kumaliza kabisa usafirishaji wa fedha
zitokanazo na uhalifu au/na fedha kwa ajili ya kufadhili ugaidi” alisema Bw.
Makombe
Aidha kanuni hizo zimeweka adhabu
zitakazochukuliwa dhidi ya wale watakabainika kutaka kupita na fedha
zinazolingana au zinazozidi kiwango kilichowekwa bila kutoa taarifa au
watakaotoa taarifa za uongo.
Alizitaja adhabu hizo kuwa ni pamoja na
kukamatwa kwa fedha taslimu walizonazo na kuchukuliwa hatua nyingine za
kisheria kama vile kufunguliwa mashtaka.
“Wahalifu pamoja na mambo mengine,
wanapenda kusafiri na fedha taslimu kwani wanaogopa kutumia benki kutuma fedha
kutokana na umakini unaoongezeka katika benki na udhaifu unaoweza kuwepo
mipakani” Alisisitiza Bw. Makombe
Kamishna huyo amewaasa washiriki wa
warsha hiyo kutekeleza jukumu hilo kwa uadilifu na uaminifu mkubwa
ili kuziba mianya yote ambayo wahalifu wanaweza kuitumia kutimiza kusudi
lao ovu na kuhatarisha usalama wa nchi.
Kutokana na umuhimu wa ushiriki wa
wadau mbalimbali katika utekelezaji wa kanuni hizo warsha hiyo imejumuisha
washiriki kutoka taasisi mbalimbali wengi wao wakiwa ni maafisa forodha.
Washiriki hao wametoka Wizara ya Fedha
na Mipango, Wizara ya Fedha na Mipango-Zanzibar, Wizara ya Mambo ya Nje,
Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kikanda, Mamlaka ya Mapato Tanzania na
vikosi vya ulinzi na usalama
Wengine ni Bodi ya Mapato Zanzibar,
Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo-Zanzibar, Shirika la Posta, Benki kuu ya
Tanzania, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka-Zanzibar, Ofisi ya Mkurugenzi wa
Mashitaka-Tanzania Bara Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania Bara na Zanzibar,
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, Idara ya uhamiaji na Kitengo cha
Kudhibiti Fedha Haramu.
Post a Comment
karibu kwa maoni