0
Rais wa Tanzania, Dk John Pombe Magufuli.
RAIS John Magufuli amefuta umiliki wa mashambapori 14 yaliyopo mkoani Morogoro yasiyoendelezwa yenye jumla ya ukubwa wa ekari 15,567.6 yakiwamo ya mfanyabiashara maarufu jijini Dar es Salaam, Jeetu Patel na la Esther Sumaye (pichani) ambaye ni mke wa Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
Aidha, serikali imesema haifuti umiliki wa mashamba kwa kuonea mtu, itikadi zake za kisiasa, dini, rangi ama kabila, bali inazingatia misingi ya kisheria iliyowekwa kwa wale wote wasioyandeleza kwa miaka mingi ikiwamo kushindwa kulipia kodi ya ardhi iliyowekwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za ardhi zilizopo.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema hayo jana katika kikao maalumu cha wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro ikiongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe pamoja za wilaya ya Kilosa na Mvomero, kilichohusu kutolewa kwa taarifa juu ya kufutwa kwa mashamba pori 14 ya mkoa huo na Rais Magufuli.
Lukuvi aliwaambia wajumbe hao kuwa Rais amefuta umiliki wa mashamba pori 14 yaliyopo mkoani humo yasiyoendelezwa yenye jumla ya ukubwa wa ekari 15,567.6, baada ya uongozi wa wilaya za Morogoro, Kilombero, Kilosa na Mvomero, kuwasilisha mapendekezo kwake kuomba kufutwa kwa mashamba pori hayo na kuyawasilisha kwa Rais.
Alieleza kuwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, wananchi wa Mkoa wa Morogoro walitoa kilio chao juu ya ukosefu wa ardhi ya kilimo kutokana na mashamba mengi kuhodhiwa na watu wachache na kushindwa kuyandeleza na wengine kuwakodishia.
Alisema baada ya Rais kuingia madarakani, alifanyia kazi mapendekeo yaliyowasilishwa na waziri baada ya kupokea kutoka viongozi wa halmashauri na mkoa huo kuhusu kufutiwa hatimiliki zao.
Alisema Rais ametekeleza jambo hilo kwa kuyafuta mashamba pori 14 yakiwemo matano ya Noble Agricultural Enterprises Ltd yaliyopo katika Kijiji cha Mvumi, Wilaya ya Kilosa lenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,661 ambayo ni ya mfanyabiashara maarufu Jeetu Patel pamoja na la mkewe Sumaye, Esther.
“Rais anapofuta hatimiliki ya mashambapori, anazingatia utaratibu wa kisheria bila kumwonea mtu kulingana na dini yake, rangi yake, kabila ama itikadi ya chama,” alisema Lukuvi na kuongeza mashamba mengi yanafutwa kwa kusababishwa na wamiliki wenyewe kwa kushindwa kufuata masharti ya ardhi yakiwemo kukosa kulipa kodi ya serikali kipindi kirefu na kutoyandeleza cha asilimia zilizotajwa na kisheria na kubakia ni mapori.
Lukuvi aliyataja mashambapori yaliyofutwa umiliki wake yakiwemo manane kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa likiwemo la Jitu na mawili kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, miongoni mwa hayo ni la Esther Sumaye lenye namba 21919 likiwa na ukubwa wa ekari 473.
Mashambapori mengine yaliyofutiwa umiliki wake ni pamoja na mashamba manne ya Noble Agricultural Enterprises Ltd yaliyopo katika Kijiji cha Mvumi Wilaya ya Kilosa lenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,661.
Lukuvi alitaja mashambapori mengine mawili tofauti yaliyokuwa yakimilikiwa na Shanta Estate Co Ltd yaliyopo Msowero pia wilayani Kilosa yenye ukubwa wa jumla ya ekari 2,200 na shambapori jingine ni lililokuwa linamilikiwa na New Msowero Farms Ltd yenye ukubwa wa ekari 1,769.
Mashambapori mengine ni la Darbrew Limited lenye ukubwa wa hekta 386.7 lililopo Msowero, shamba lililokuwa linamilikiwa na James Longido, Saidi Longido, Lengai Lupejo, Sefu Longido na Maboli Sangati yenye ukubwa wa hekta 224. 62 yakiwa katika Kijiji cha Wami Luhindo wilayani Mvomero.
Waziri Lukuvi pia alitaja mashamba mengine yasiyoendelezwa yaliyofutiwa hatimiliki na Rais ni Nguru ya Ndege Morogoro lililokuwa likimilikiwa na Guard Kiangi lenye ukubwa wa ekari 100 pamoja na shamba lenye hekta 192.12 lililopo eneo la Wami Luhindo, Mvomero ambalo lilikuwa likimilikiwa na Ndeshukurwa Sumari.
Mashambapori mengine yaliyofutwa umiliki wake ni Sangasanga Morogoro lililokuwa linamilikiwa na Leila Omari lenye ukubwa wa ekari 326 na jingine ni la Usafirishaji Mikoani Union Ltd lenye ukubwa wa ekari 6,010 lililipo katika Kijiji cha Ruipa Wilaya ya Kilombero.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe alisema mkoa huo una mashambapori 223 na kati ya hayo, 198 yapo katika Wilaya ya Kilosa na kwamba kazi ya kuainisha inaendelea kufanywa na timu ya wataalamu wa mkoa huo ili yawasilishwe kwa waziri mwenye dhamana.
Hata hivyo, alitoa onyo kwa wananchi kuacha kuyavamia mshamba pori yaliyofutiwa umiliki wake na Rais na badala yake wasubiri utaratibu utakowekwa na serikali ya mkoa na halmashauri za wilaya husika kwa mujibu wa sheria ili kuweka matumizi bora ya ardhi kwa manufaa ya watu wa nchini.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top