0
Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.
SERIKALI imewataka wawekezaji waliopewa maeneo kwa ajili ya kilimo cha miwa, waanze uzalishaji wa sukari mara moja. Hayo yamesemwa jana na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwaijage wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Mwijage alisema nchi inapaswa kuruhusu sukari kutoka Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuingia bila kulipa kodi, lakini wameomba walipishe kodi sukari hiyo kwa sababu sekta ambayo inaajiri watu wengi ni sukari, hivyo wameona wakiruhusu sukari kutoka nchi hizo ziingie, viwanda ambavyo ni vichanga vitashindwa kukua hivyo walikubali sukari kutoka SADC iingie na watalipa kodi.
Alisema Tanzania ina uwezo wa kuzalisha 200,000, lakini kama viwanda vikiboreshwa na vikasimamia vizuri, uwekezaji katika mashamba ya sukari, utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni mbili kwa hiyo kwa wale walioomba maeneo ya kuanza utaratibu wa kuwekeza nafasi iko wazi wawekeze.
“Sukari ambayo inayotoka SADC itakuwa inatozwa ushuru wa asilimia 25 hivyo sukari itakuwa inaagizwa kwenye nchi hizo ambazo ziko kumi na tano na siyo sehemu nyingine,” alieleza Mwijage na kuongeza: “Hatujavitaifisha viwanda ila tunachokifanya ni kuvichukua na kuwapa watu wengine ili waviendeleze, lengo letu ni kuifanya nchi hii iwe na viwanda ambavyo vinakuwa na uwezo wa kuzalisha tofauti na kuwa na viwanda ambavyo ni hewa,” alisema.
Aliongeza kuwa mkakati wa viwanda vya SADC una nguzo tatu, ambazo ni uendelezwaji kwa njia ya kuleta mageuzi ya kiuchumi, kukuza ushindani na kuongeza utangamano wa kikanda.
Aidha, alisema pia mkakati huo umeainisha maeneo makuu ambayo nchi za SADC zinaweza kuyatumia katika kukuza ushiriki wao kwenye mnyororo wa thamani na hivyo kuongeza ushiriki wa nchi hizo kwenye masoko ya kikanda na kimataifa.
Alisema uzalishaji wa viwanda ulipo ndani ya nchi husika kwa kulingana na nchi za SADC kwa kufuata vigezo vilivyowekwa, Tanzania imekuwa na ushindani mzuri katika maeneo ya usindikaji mazao ya kilimo, shughuli zinazoendana na uchenjuaji madini, dawa za binadamu na uzalishaji bidhaa zinazotumiwa mara kwa mara pamoja na utoaji huduma wa bidhaa za uwekezaji mashine na vifaa.
Aidha, alisema sekta ya viwanda imepokea Euro milioni 1.4 kwa ajili ya kulenga zao la alizeti. Alieleza kuwa wanataka kuongeza ubora katika kilimo hicho kwa sababu asilimia kubwa ya mafuta ya alizeti huwa yanauzwa nje ya nchi na yanapendwa zaidi, hivyo lengo ni kuimarisha kilimo hicho pia.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top