0

Wakati Rais John Magufuli akitoa ajira mpya 3,000 jeshini, Mkuu wa Majeshi (CDF), Jenerali Venance Mabeyo amewataka wanajeshi kutojihusisha na matumizi mabaya ya mitandao kwa kuwa ni kinyume na kanuni za ulinzi wa Taifa.
Ajira hizo mpya ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwa na jeshi imara na la kisasa ili litakalofanya kazi ya ulinzi wa nchi kwa ufanisi.
Akizungumza baada ya kutunuku kamisheni kwa maofisa 422 wa JWTZ kundi la 61, Rais Magufuli alisema lengo la nafasi hizo ni kuhakikisha jeshi linakuwa na askari wa kutosha.
Alisema, “Jeshi haliwezi kuwa na maofisa tu, tutaongeza na askari wa kawaida, wengi watakaopata nafasi hizi nataka wawe wamepitia JKT, tunataka tujenge jeshi la kisasa. Kuhusu changamoto ndogondogo msiwe na wasiwasi tutazishughulikia na wiki ijayo tutaanza kufanyia kazi madai yenu.”
Rais Magufuli alisema utawala wake umekuwa na imani kubwa na jeshi ndiyo sababu amekuwa akiwateua wanajeshi katika nafasi mbalimbali za uongozi ili walete maendeleo kwa haraka.
“Nilipoingia madarakani na kuanza kuteua wanajeshi katika nafasi mbalimbali kuna watu walianza kunishangaa na wapo ambao walisema nataka kuifanya nchi ya kijeshi. Nawapenda wanajeshi kwa sababu wanapeleka mambo kwa haraka, ndiyo sababu niliwateua ili mambo yaende kasi na ninaona jinsi wanavyochapa kazi na kupeleka mambo harakaharaka.”
Mbali ya suala hilo la ulinzi, Rais Magufuli pia alizungumzia mambo mengine ya kimaendeleo akiwataka Watanzania kuacha kujihusisha na kilimo cha bangi na badala yake wajikite kwenye kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Alisema dawa za kulevya zinawaharibu vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa hali inayosababisha wengi wao kushindwa kufanya kazi.
“Hatuwezi kuwa tunatengeneza Taifa la watoka udenda. Hao hata uwape kazi gani hawataweza kufanya. Ukimpeleka kiwandani mashine zinaweza kumkata mikono, vijana acheni masuala ya madawa ya kulevya ni lazima tutengeneze Taifa lenye mwelekeo ili siku moja Tanzania iwe nchi ya kutoa misaada.”
Aliwasisitiza wakazi wa Arusha kuendelea kuchapa kazi na kutokubali kutumiwa na wanasiasa kwani maendeleo hayana chama.
“Msikubali kuyumbishwa na itikadi za vyama, tushikamane kuleta maendeleo na kutunza amani yetu. Wengine wanawapa viroba mnaandamana ndiyo sababu tumeamua kuviondoa, vijana mchape kazi. Mimi naweza kusimama na kusema Chadema oyee na nikaweka vidole kwa ishara wanayoweka kwani nitapungukiwa nini! Hizo alama hazina faida kama una njaa,” alisema.
Kuhusu mwenendo wa uchumi Rais Magufuli alisema Tanzania imeanza kubadilika na kasi yake ya ukuaji uchumi inaifanya kuwa miongoni mwa nchi tatu za Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa haraka.
“Wanaolalamika hela hakuna ni wezi. Sasa hivi mzunguko wa fedha umekaa vizuri, hapo awali zilikuwa nyingi mtaani kwa sababu zilikuwa za wizi lakini sasa thamani yake inaonekana, najua tunavyopambana hivi kuna watu hawapendi wanaumia kwa sababu walikuwa wakila jasho la Watanzania.
“Nimeamua niwe sadaka ya Watanzania kwa ajili ya kuwanyoosha mafisadi. Hamjui mateso ninayopitia, ni shida kuwa Rais, nimeyaona mateso kuwa Ikulu, niliomba kwa kujaribu nikasukumwa huko. Sababu niliingia bila kutoa rushwa lazima nifanye kazi kwa ajili ya Watanzania hakuna fisadi aliyenichangia hela hivyo sitaogopa kumtumbua yeyote na nitawatumbua kwelikweli.”
Kuhusu kwenda nje ya nchi Rais Magufuli alirejea kauli yake kwamba amepata mialiko mingi kutoka kwa mashirika na wadau mbalimbali wa maendeleo lakini haendi kwa sababu anafanya kazi ya kujenga nchi.
“Kila mara wananialika nimeshaacha mialiko karibu 60. Niende huko kufanya nini? Nasafisha kwanza hapa, nikienda huko kutaharibika, nasafisha nyumba yangu, niliomba urais wa Tanzania siyo wa kutembelea nchi za watu. Kama kutembea nilitembea wakati nasoma nchi zote hizo nilifika sasa nimeamua kuchapa kazi. Fedha nyingi za Watanzania zilitumika kwenye safari, kuna watu walikuwa hawatulii wanapishana tu angani.”
Kuhusu Serikali kuhamia Dodoma, Dk Magufuli alisema anataka ifikapo mwakani watumishi wote wa umma wawe wamehamia makao makuu ya nchi.
“Nimesema watu wahamie Dodoma, mimi mwenyewe naenda mwaka kesho... sasa atakayebaki Dar abaki na kazi hamna. Nashangaa kwa nini hawataki kwenda Dodoma wakati tumejenga barabara nzuri.”
Jenerali Mabeyo
Awali, Jenerali Mabeyo aliwataka maofisa hao waliotunukiwa kamisheni kufanya kazi kwa uzalendo, utii, kuheshimu na kulinda Katiba ya nchi.
“Kutunikiwa kamisheni ni ishara ya kupewa dhamana ya uongozi, niwasihi sana kuheshimu, kuthamini na kuzingatia kiapo cha utii mlichoapa leo mbele ya Amiri Jeshi Mkuu. Mkumbuke kiapo hiki ndicho kinacholinda Sheria ya Ulinzi wa Taifa ambayo ndiyo imetoa kanuni za ulinzi wa Taifa.
“Bahati mbaya wapo baadhi ya maofisa na askari wanaosahau haraka na kuanza kukiuka kiapo chao, naomba urejee matamshi uliyoyatoa leo, yanaelekeza wajibu wako, utii, kuilinda Katiba pamoja na kumtii Rais.”
Kuhusu matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, Jenerali Mabeyo alisema kumekuwapo na baadhi ya wanajeshi wanaojihusisha na vitendo hivyo vinavyokiuka kanuni na taratibu za JWTZ.
“Wajibu wa kwanza wa jeshi letu ni kuilinda nchi, wananchi na mali zao, tuwe macho na matishio yaliyopo katika zama hizi ambayo yanatoka ndani na nje ya nchi, ni vyema tukayaona hayo na kuwa tayari kukabiliana nayo mahali popote na wakati wote.
“Endeleeni kuwa na uzalendo, imarisheni uhusiano mzuri na wananchi, epukeni kwa namna yoyote ile kuliingiza jeshi kwenye siasa kwani kufanya hivyo ni hatari kwa ustawi wa Taifa letu,”
Jenerali Mabeyo alisisitiza kuwa nchi iko salama na kuwataka Watanzania wote kuwa tayari kuilinda nchi yao kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top