0









WAKATI Ofi si ya Bunge ikisisitiza kuwa fedha zilizochangwa na
wabunge kiasi cha Sh milioni 43 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), tayari zimetumwa katika
akaunti ya Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa matibabu, Benki
Kuu ya Tanzania (BoT) imeingilia kati.

Kwa sasa Lissu anaendelea na matibabu nchini Kenya baada ya
kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana mkoani Dodoma, Septemba 7,
mwaka huu.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari,
Elimu kwa Umma na Mawasiliano cha Bunge kwa vyombo vya habari jana,
fedha hizo zimetumwa kupitia BoT.

Taarifa hiyo ilisema kwa mujibu wa viwango vya kubadilishia fedha vya
BoT kwa siku hiyo wakati fedha hizo zikitumwa ilikuwa ni sawa na
Shilingi za Kenya 1,977,120.58. Ofisi ya Bunge imeeleza kuwa kiasi hicho
cha fedha kilitumwa siku ya Septemba 20, mwaka huu kwenda Benki ya
Barclays, tawi la Hurlringham, kwenye akaunti namba 0451155318 yenye
jina la Kenya Hospital Association.

Taarifa hiyo iliambatanisha barua yenye kumbukumbu, Ref.NO
FA.93/155/01B/260 kutoka kwa Meneja wa Akaunti za Nje wa BoT
inayothibitisha benki hiyo kutuma fedha hizo kwa akaunti hiyo ya
hospitali anakotibiwa Lissu. Ofisi hiyo ya Bunge imelazimika kutoa
ufafanuzi huo baada ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe
alipozungumza na waandishi wa habari hivi karibuni, kulitupia lawama
Bunge na hasa akielekeza tuhuma zake kwa Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai
kuwa wabunge wamekatwa posho kuchangia gharama za matibabu ya Lissu,
lakini fedha zilizopatikana hazikuwa zimekabidhiwa.

Hata hivyo, Spika Ndugai alimjibu Mbowe na kumtaka aache kupotosha
taarifa za ushiriki wa Bunge katika tiba ya Lissu na kulichukuliwa suala
hilo kisiasa. Alifafanua kuwa ni utaratibu wa kawaida kwa Bunge au
ofisi inayotumia bima, iwapo inataka mgonjwa wake kuhamishiwa hospitali
nyingine, lazima itoe taarifa ya daktari inayoelezea kuhamishwa kwa
mgonjwa huyo.

Aidha, Ndugai alimtaka Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani
Bungeni kukubali ofa ya serikali ya kutaka kugharamia tiba za Lissu
akiwa nje ya nchi. Kwa sasa matibabu ya Lissu yanatokana na michango ya
wadau mbalimbali ambapo kwa mujibu wa Mbowe hadi juzi jumla ya Sh
milioni 204 zilikusanywa ambazo hata hivyo alibainisha kuwa hazitoshi na
michango inaendelea. Kwa mujibu wa msemaji wa familia ya Lissu, Alute
Mughwai, hali ya mbunge huyo inaendelea kuimarika na kwamba aliweza
kuzungumza naye kwa kutumia simu ya kiganjani na kuwashukuru Watanzania
kwa sala na michango yao.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top