Septemba 7, 2017, Dodoma: Serikali imeahidi kuendelea kuboresha mifumo ya kukusanya
mapato pamoja na kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii ili kuleta unafuu
wa maisha ya Wastaafu na Wananchi kwa ujumla.
Hayo yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa
akijibu swali la msingi la Mbunge wa Mtambile Mhe. Masoud Abdallah Salim (CUF),
aliyetaka kujua mpango wa Serikali katika kuboresha mafao ya uzeeni ili kuondoa
malalamiko ya hali ngumu ya maisha wanayoishi Wastaafu.
Mhe.
Salim alisema kuwa kumekuwepo malalamiko
mengi kutoka kwa Wastaafu ambao wakati wa utumishi wao walilitumikia Taifa kwa
uwaminifu na uadilifu mkubwa, kuhusu kuishi maisha magumu yanayotokana na
kucheleweshewa mafao yao ya uzeeni yasiyolingana na kupanda kwa gharama za
maisha.
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, Serikali kwa sasa imejielekeza zaidi
katika kuboresha miundombinu ya usafiri
na usafirishaji, nishati ya umeme, maji, huduma za afya, elimu na kiuchumi hususan
katika ukusanyaji mapato kwa lengo la kuboresha maisha ya Wastaafu na Wananchi
kwa ujumla.
“Tuendelee
kuiunga mkono Serikali yetu katika juhudi zake za kujenga uchumi imara, uchumi
wa viwanda ambao ndio msingi mkuu wa kuimarisha mapato ya Serikali”. Alisema
Dkt. Kijaji.
Alisema
kuwa maboresho ya viwango vya pensheni kwa Wastaafu yasiyoendana na maboresho
ya miundombinu ya kiuchumi na huduma za kijamii hayawezi kuondoa malalamiko ya
Wastaafu hivyo Serikali imelenga zaidi kutatua changamoto za kiuchumi na
kijamii ili kupunguza malalamiko hayo.
Dkt.
Kijaji alifafanua kuwa nyongeza ya pensheni kwa Wastaafu, mishahara na maslahi
mazuri kwa Watumishi wa Umma itaongezeka kama mikakati na azma ya Serikali ya
kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi itafanikishwa.
Aidha Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali
inatambua umuhimu wa kuboresha viwango vya pensheni ili kukidhi mahitaji muhimu
ya Wastaafu, kwa kutambua hilo Mwezi Julai 2015, Serikali iliboresha kiwango
cha pensheni kutoka Sh. 50,114 hadi Sh. 100,125 kwa mwezi.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
Post a Comment
karibu kwa maoni