0



Aliyekuwa Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta ,ametoa msimamo wake juu ya uamuzi wa mahakama uliotolewa leo wa kurudiwa kwa uchaguzi wa urais, na kusema kuwa hakubaliani nao ingawa anaheshimu uamuzi huo.
Akizungumza katika Ikulu ya Kenya muda mfupi baada ya uamuzi wa mahakama kutolewa, Uhuru Kenyatta amesema anaheshimu uamuzi uliotolewa na mahakama wa kufuta matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi, lakini hakubaliani na uamuzi huo.
“Hii ni muhimu kwetu kama Wakenya kuheshimu uamuzi wa sheria, binafsi sikubaliani na uamuzi uliofanywa leo, lakini naheshimu”, alisema Uhuru Kenyatta.
Uhuru Kenyata aliendelea kwa kusema kwamba “kama ambavyo nilisema mamilioni ya Wakenya walisimama kwenye mstari, wakafanya uamuzi wao, lakini watu 6 wamekwenda kinyume, nyinyi kama wakenya mliamua na kuwachagua kwa wingi viongozi wa Jubilee, mahakama wamefikia uamuzi tunauheshimu na hatukubaliani nao”, alielezea.
Pamoja na hayo Uhuru Kenyatta amesema kwa kuwa wanaheshimu uamuzi wa mahakama, wako tayari kurudi kwenye kampeni na kupiga kura tena kama ambavyo mahakama imetaka.
“Hatupo vitani na kaka zetu, nyinyi mjipange na sisi tunajipanga, tuko tayari kurudi kuongea na wakenya kuwaambia yale tunataka kufanya, tafadhali acheni ukabila, acheni utengano uzeni sera mshindane na zetu, acha Wakenya waamue, watu 6 hawawezi badilisha nia ya wananchi milioni 40, Wakenya ndio wataamua “, alisema Uhuru Kenyatta.
Uhuru Kenyatta hakuishia hapo aliendelea kwa kuwasihi wakenya kudumisha amani, bila kujali itikadi za vyama na ukabila, ili kuendelea kuijenga Kenya iliyo bora.
“Na tena Wakenya wenzangu nasema amani, jirani yako atabaki kuwa jirani yako, tupo tayari kurudi kwa wananchi na ajenda hiyo hiyo tuliyo wapelekea watu wetu ya kujenga umoja wa nchi yetu, sisi ni kitu kimoja, sisi ni jamii ambayo inaitwa Wakenya na hivyo ndivyo itakuwa”, alisema Uhuru Kenyatta.
Leo asubuhi Makama ya juu zaidi ilitoa uamuzi wa kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na muunganiko wa vyama vya upinzani nchini Kenya (NASA) dhidi ya Tume ya Uchaguzi iliyosimamia uchaguzi huo ambao Uhuru Kenyatta aliibuka mshindi, na kuamua kufuta matokeo hayo huku ikitaka urudiwe baada ya siku 60.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top