
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla leo Ijumaa ametangaza
kusitishwa operesheni zilizokuwa zinaendelea katika pori tengefu la
Loliondo na ametaka mifugo yote inayoshikiliwa na Hifadhi ya Taifa ya
Serengeti ambayo haijafikishwa mahakamani kuachiwa.
Akizungumza
katika mkutano wa hadhara katika mji wa Wasso Loliondo baada ya
kukutana na kamati ya ulinzi na usalama na madiwani, Dk Kigwangalla
amesema amechukua uamuzi huo ili kusimamia dhana na uhifadhi endelevu na
shirikishi.
Amesema
wizara hiyo itaendelea kusimamia sheria za uhifadhi kwa kushirikiana na
jamii na haitakubali watu wachache kuvunja sheria za uhifadhi.
"Kwa
mamlaka niliyonayo kwa watendaji wote wa wizara walio chini yangu,
natangaza kusitisha operesheni iliyokuwa inaendelea na kurejeshwa kwa
wananchi mifugo yote iliyokuwa inashikiliwa na wahifadhi ambayo uamuzi
wake, hausubiri Mahakama," amesema.
Waziri
Kigwangalla pia aliagiza wataalam wa maji katika Halmashauri ya
Ngorongoro, kushirikiana na wataalam wa hifadhi kutoa maeneo nje ya
hifadhi ili mifugo ya wananchi ipate maji.
Hata hivyo, amesema ili kudhibiti mifugo ya nchi jirani, kuingia
katika maeneo ya hifadhi nchini, mifugo yote sasa inatakiwa kuwekwa alama na mifugo kutoka nje itakayokamatwa itataifishwa.
Waziri
Kigwangalla amesema anataka mamlaka ambazo zipo chini yake, kurejea
katika kazi ya msingi kuhifadhi na kupambana na ujangili badala ya
kufanya kazi ya kuchunga mifugo inayokamatwa.
"Uchukuaji
mifugo inawafilisi wananchi na inajenga uadui baina ya wahifadhi na
wananchi...kuna mifugo inakamatwa inakaa muda mrefu katika hifadhi
baadhi inakufa na mingine inachungwa hifadhini, jambo ambalo sio wajibu
wa wahifadhi," amesema.
Akizungumzia
mifugo mingine ya wananchi, iliyokamatwa maeneo mengine ya hifadhi
nchini, Dk Kigwangalla alitoa siku saba kwa watendaji wa wizara yake
kumpa mapendekezo ya namna bora ya kutatua tatizo hilo ili afanye
maamuzi.
Post a Comment
karibu kwa maoni