0
MNYAMA faru aliyepewa jina la Spika wa Bunge, Job Ndugai ameanza vurugu katika Hifadhi ya Ngorongoro hususan ndani ya kreta.
Spika Ndugai aliwahi kuwa Mhifadhi na Mjumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA). “Faru wote zaidi ya 60 wanaishi ndani ya Kreta la Ngorongoro, lakini hivi karibuni ‘Faru Ndugai,’ amekuwa ni pasua kichwa, kila mara anatoroka kutoka bondeni na kupanda maeneo ya nyanda za juu za Hifadhi ya Ngorongoro na kuwapa wakati mgumu askari wanyamapori na wahifadhi wengine,”
Hillary Mushi, Meneja wa Kitengo cha Wanyamapori Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) alisema jana. Mushi alisema kuna usalama zaidi ndani ya Bonde la Ngorongoro ambalo liko chini ya darubini za wahifadhi kwa saa 24.
Hatua ya ‘Faru Ndugai,’ kutoroka kreta kila mara inahatarisha maisha yake kwani faru wanawindwa na kuuawa zaidi duniani. Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Ngorongoro, Daktari Freddy Manongi, vitendo vya ujangili vimedhibitiwa kwa kiasi kikubwa katika himaya yake.
Inadaiwa ushindani mkubwa na vita vya mara kwa mara ya faru dume waliomo kreta kugombea majike ndio chanzo cha Faru Ndugai kutoroka kila mara bondeni humo. Wakati huo huo, afya ya Faru Mzee kuliko wote duniani yaani ‘Faru Fausta’ ambaye yuko chini ya ulinzi maalumu katika Bonde la Ngorongoro, nayo inaendelea kuimarika baada ya mnyama huyo kupona majeraha na kurejesha nguvu ya mwili.
“Kwa sasa ‘Fausta,’ mwenye miaka 55 amepona lakini kwa sababu ya umri mkubwa, macho yake yanakosa nguvu ya kuona vizuri ndio maana tumemweka ndani ya banda maalum ili asishambuliwe na fisi,” alisema Daktari wa Wanyama wa NCAA, Athanas Nyaki.
Kwa mujibu wa wataalamu, kawaida Faru ana uwezo wa kuishi kati ya miaka 35 na 40, lakini ‘Bibi Fausta,’ amevunja rekodi ya kufikisha miaka 55 na anaendelea kuishi. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeanzisha shamba maalumu kuotesha majani yenye virutubisho na tiba asili kwa wanyama jamii ya faru.
“Majani hayo, ‘Lusini’ (Leucaena) ya jamii ya mikunde yana protini nyingi zinazosaidia kujenga misuli kwa wanyama haraka na ndiyo yalimsaidia Faru Fausta kupona haraka,” aliongeza Nyaki.
Awali, Meneja wa Kitengo cha Wanyamapori, Mushi alieleza walikuwa wakiagiza majani hayo kutoka Kenya kwa gharama za Sh milioni tano kwa mzigo mmoja. “Mbali na gharama za kununua haya majani kutoka shamba la ‘Lord Dalamere,’ kule Naivasha, tulilipia usafiri na vibali Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Mapato (TRA), Tume ya Mionzi (TAEC) na Idara ya Uhamiaji,” alisema Mushi.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top