#Anaandika Benny Mwaipaja.
Serikali
imelipa madeni ya wazabuni, wakandarasi na malimbikizo ya wafanyakazi
yanayofikia kiasi cha shilingi bilioni 190 katika kipindi cha miezi mitatu
kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu baada ya kufanya uhakiki wa madeni halali
inayodaiwa na wafanyakazi na watoa huduma mbalimbali.
Hayo
yamesemwa Mjini Bukoba mkoani Kagera na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe.
Dokta Ashatu Kijaji (Mb), wakati akizungumza na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa
mkoa huo akiwa katika ziara ya kikazi kukagua utendaji wa Mamlaka ya Mapato
Tanzania (TRA) na Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA).
Dokta
Kijaji alisema kuwa wazabuni wamelipwa kiasi cha shilingi bilioni 67.2,
wakandarasi wamelipwa shilingi bililioni 24.2, watoa huduma mbalimbali wamelipwa
Shilingi bilioni 38, watumishi wa umma wamelipwa Shilingi bilioni 37, huku
wadai wengine wakilipwa shilingi bilioni 24.
Alisema
kuwa katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi
trilioni 1 kwa ajili ya kulipa madeni mbalimbali na kwamba itaendelea kulipa
madeni yote yaliyohakikiwa.
Dkt.
Kijaji aliiambia Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera kwamba Serikali
inatambua mchango wao mkubwa katika maendeleo ya Taifa kutokana na kulipa kodi
zinazochangia kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za jamii.
Alitoa
wito kwa wafanyabiashara kutumia mashine za kielektroniki katika biashara zao,
kutoa stakabadhi wanapouza bidhaa na huduma huku wananchi wakiaswa kudai
stakabadhi wanapofanya manunuzi ya aina yoyote na kuhakikisha kuwa stakabadhi
hizo zinaonesha kiasi halisi walicholipia huduma na bidhaa walizonunua.
Akizungumza
kwaniaba ya Jumuiya ya Wafanyabiashara mkoani Kagera, Mwenyekiti wa Jumuiya
hiyo Bw. Seif Mkude, alipongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna
inavyohamasisha na kushikia bango masuala ya kodi kwa manufaa ya Taifa.
Alisema
kuwa wafanyabiashara wameridhika na namna kodi wanazolipa zinavyosimamiwa
kikamilifu na kutekeleza miradi dhahiri ya maendeleo na kuahidi kuwa wataendelea
kulipa kodi hizo ili kujenga uchumi wa nchi.
Alitoa
wito kwa wafanyabiashara wenzake kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuunga
mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli huku akiishauri
Serikali kuondoa kero ndogondogo zilizotolewa na wafanyabiashara wakati wa
mkutano huo.
Akizungumza
kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, Mkuu wa wilaya ya Bukoba Bw. Deodatus
Kinawiro, aliwashauri wafanyabiashara hao kupanua wigo wa biashara zao ili
waweze kunufaika na uwepo wa soko huru katika nchi zaidi ya nne zinazopakana na
mkoa huo ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi, DRC Kongo, Kenya na nchi nyingine.
Post a Comment
karibu kwa maoni