#Anaandika Benny Mwaipaja, Kagera
NAIBU waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji, ameziagiza Mamlaka na Taasisi zote za Umma kufanya
ununuzi wa vifaa na mafuta kupitia Wakala wa Serikali wa ununuzi na ugavi
(GPSA) kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge na kuwaonya wahusika wote watakaoendelea
kukaidi maagizo hayo kwamba watachukuliwa hatua za kisheria.
Dkt. Kijaji ametoa maagizo
hayo mkoani Kagera baada ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na
Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoani humo na kubaini kuwa taasii na idara
nyingi za umma zinafanya manunuzi nje ya mfumo wa GPSA jambo ambalo amesema ni
ukiukwaji mkubwa wa sheria.
Alisema kuwa lengo la
Serikali la kuanzishwa kwa wakala huo pamoja na mambo mengine ilikuwa kudhibiti
matumizi ya Serikali na kuonya kuwa Serikali haitakubali kuona sheria
zinakiukwa kwa makusudi na kwa malengo yanayoonesha kuna nia isiyo njema katika
matumizi ya fedha za umma.
“Hili si ombi ni maelekezo
na ni agizo, taasisi zote zipate huduma kutoka kwa wakala wetu (GPSA) kwani
Serikali ilikuwa na dhamira ya uwepo wa matumizi sahihi ya fedha za matumizi
wanazopelekewa na ndiyo maana ukaanzishwa Wakala huu” Alisema Dkt. Kijaji
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba,
Deodatus Kinawiro, akizungumza kwaniaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, aliiagiza
Wakala wa Ununuzi na Ugavi (GPSA) mkoani humo kumpelekea orodha ya taasisi
ambazo hazitumii huduma za wakala huo ili aweze kuchukua hatua.
Alisema kuwa ni jambo
lisilofaa kwa Taasisi za Umma kukiuka sheria na kwamba watatekeleza maelezo
yaliyotolewa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango haraka ili kuokoa fedha za
Serikali na kuweka uwajibikaji.
Awali, Kaimu Mkuu wa
Wakala wa Ununuzi na Ugavi GPSA mkoa wa Kagera Bi. Dorothea Bugenyi alieleza
kuwa katika kipindi cha miaka 3 iliyopita Wakala huo umeongeza makusanyo
yatokanayo na mauzo ya vifaa na mafuta kutoka Shilingi bilioni 1.9 hadi kufikia
Shilingi bilioni 2.34.
Alisema kuwa mapato hayo
yangekuwa makubwa zaidi endapo taasisi zote za umma zingetii sheria na kufanya
manunuzi yao ya vifaa na mafuta kutoka kwa Wakala huo na kuiomba Serikali
kuusaidia Wakala huo kuziagiza taasisi zake za umma kutekeleza sheria hiyo kwa
vitendo.
Post a Comment
karibu kwa maoni