0
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey PolepoleHALMASHAURI Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) kimetangaza majina ya wanachama walioomba nafasi za uongozi wa chama hicho kwenye ngazi mbalimbali ikiwemo za Jumuiya za Chama.
Imeelezwa kuwa jumla ya wanachama 3,004 waliomba kuteuliwa ili wakagombee nafasi 261 za uongozi ndani ya Chama. Akizungumza na Vyombo vya Habari kwenye Ofisi ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliwataja baadhi ya viongozi waliopitishwa kwenye nafasi za unyekiti wa Jumuiya za chama hicho akiwemo aliyewahi kuwa Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka.
Kwa mujibu wa Polepole, waliopitishwa na NEC kugombea nafasi ya Uenyekiti wa wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT) ni Gaudencia Kabaka, Dk Juliana Manyerere, Sophia Mpumilwa na Ngoro Malenya.
Kwa upande wa Jumuiya ya Wazazi, waliopitishwa ni Dk Edmund Mndolwa, Barton Kihaka, Simon Lububu na Fadhili Maganya. Wanachama wengine waliopitishwa kugombea uenyekiti kwa upande wa Umoja wa Vijana (UVCCM) ni Hery James, Kamana Simba, Juma Mtoro, Mganwa Nzota, Thobias Richard, Simon Kipara na Juma Mwaipaja.
Polepole alisema kuwa Mikutano Mikuu ya Jumuiya ngazi ya mikoa kwa ajili ya uchaguzi wa wanachama waliopitishwa na NEC itafanyika tarehe 27 hadi 30 mwezi huu, wakati Mikutano Mikuu ya CCM ya Mikoa itafanyika tarehe 2 hadi 5 mwezi ujao.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM alisema kuwa CCM ina hazina kubwa ya viongozi na akawataka wanachama ambao hawakupitishwa na NEC kuendelea kuwa watulivu na kuendelea kukitumikia Chama kwa uaminifu. Alisema CCM ina wanachama zaidi ya milioni 12 na ndiyo maana zilipotangazwa nafasi za uongozi walijiotokeza wanachama 3,004. Alisema hata kwa wanachama walioomba ujumbe wa Halmashauri Kuu walikuwa 531 wakati nafasi zilizopo ni 30 tu.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top