0
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibroad Slaa.RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli amemteua Dk Wilbrod Slaa kuwa Balozi kuanzia jana.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema kwamba Dk Slaa ataapishwa baada ya taratibu kukamilika. Dk Slaa alizaliwa Oktoba 29, 1948 na kupata elimu yake ya msingi katika shule ya Kwemusi wilayani Mbulu kuanzia mwaka 1958 hadi 1961.
Baadaye alijiunga na Shule ya Msingi Karatu kwa masomo ya darasa la tano hadi la nane mwaka 1962 hadi 1965. Baada ya hapo alijiunga na shule ya Seminari ya Katoliki ya Dung’unyi kwa masomo ya sekondari ya Katoliki ya Dung’unyi kwa masomo ya sekondari ya kidato cha kwanza hadi cha nne na baadaye akahitimu elimu yake ya kidato cha sita Seminari ya Itaga.
Alipata elimu yake falsafa kwenye Seminari Kuu ya Kibosho mkoani Kilimanjaro na baadaye masomo yake ya theolojia kwenye Seminari Kuu ya Kipalapala mkoani Tabora. Dk Slaa (pichani) alianza kazi ya upadre mwaka 1977 kwenye Kanisa Katoliki Jimbo la Mbulu.
Katika maisha yake ya upadre aliwahi kuteuliwa kuwa Msaidizi wa Askofu wa Jimbo hilo na baadaye akachaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) mwaka 1986 hadi 1991.
Dk Slaa aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha TANU Tawi la Kipalapala kuanzia mwaka 1974 hadi mwaka 1977. Katika kipindi hichohicho pia alishika wadhifa wa Katibu wa Umoja wa Vijana wa TANU.
Mbali na nafasi hizo, Dk Slaa pia aliwahi kuwa Katibu wa Tawi la CCM nje ya nchi (Rome) kuanzia mwaka 1980 hadi 1982. Baada ya kuacha wito wake wa upadre, alifanya kazi na Chama cha Wasioona kama Mkurugenzi Mtendaji kuanzia mwaka 1991 hadi 1995.
Mwaka 1995, Dk Slaa alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha ubunge kwa tiketi ya CCM ingawa baadaye jina lake lilienguliwa na vikao vya juu vya CCM. Baada ya hapo aliamua kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Katika Uchuguzi Mkuu wa mwaka 1995 alishinda nafasi ya ubunge wa Karatu na aliendelea kuwa Mbunge wa Jimbo hilo hadi mwaka 2010 alipoamua kujitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais kabla ya kujiondoa Chadema kwenye uchaguzi mkuu uliopita. Pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema kuanzia mwaka 1998 hadi 2002 na baada ya hapo akawa Katibu Mkuu wa Chama hicho

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top