0

Rais John Magufuli akitoa maelekezo kuhusu magari zaidi ya 50 yanayodaiwa kuwa ya Polisi yaliyopo bandari ya Dar es Salaam tangu mwaka 2015 kwa sababu ya kutolipiwa ushuru alipofanya ziara ya kushtukiza jana.

RAIS John Mafufuli ametoa siku saba kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) na Jeshi la Polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 na magari ya Jeshi la Polisi 53 kukwama Bandari ya Dar es Salaam kwa miaka miwili sasa huku baadhi yakiwa yamedaiwa kuingizwa kwa jina la Ofisi ya Rais wakati yeye hajui.
Jana, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya kutunzia magari ndani Bandari ya Dar es Salaam na kubaini uwepo wa magari madogo ya kubebea wagonjwa 50 ambayo yamekwama bandarini hapo tangu Juni, 29, 2015 na magari ya Jeshi la Polisi 53 ambayo yamekwama tangu Juni 2016. Dk Magufuli pia amebaini uwepo wa magari yaliyotekelezwa bandari hapo kwa zaidi ya miaka 10 hali inayopunguza uwezo wa bandari kuhifadhi mizigo.
Kutokana na hali hiyo, ametoa siku saba kwa TRA, TPA na Jeshi la Polisi kumpa taarifa juu ya sababu za magari hayo kukwama bandarini hapo kwa muda mrefu na kinyume cha sheria na kumtaja mmiliki wake na pia ameagiza magari yote ambayo yamekaa bandarini hapo kwa muda mrefu yaondolewe kwa taratibu za kisheria na kwa uwazi kutoa nafasi zaidi.
“Nataka magari yote yaliyokaa muda mrefu kupita muda uliopangwa kisheria yaondolewe haraka, kama ni kupigwa mnada yapigwe mnada, kama ni kuchukuliwa na Serikali yachukuliwe, hatuwezi kuendelea kutunza magari ya watu humu kwa miaka 10 tena watu wengine hawajulikani,” aliagiza Rais Magufuli.
Rais Magufuli pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Kamishna wa Polisi, Valentino Mlowola kuchunguza magari yote yaliyokwama bandarini baada ya kuagizwa kwa majina ya taasisi za Serikali (Rais) na kuwabaini walioshiriki katika uingizaji.
Rais Dk Magufuli aliyeongozana na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango aliwataka mawaziri hao kufuatilia utendaji kazi wa vyombo na taasisi wanazozisimamia na kuchukua hatua wanapobaini mambo yasiyofaa.
Pia Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali Simon Sirro kuyakagua magari 53 ya Polisi ambayo yamekaa muda mrefu bandarini bila kutolewa. Alimtaka IGP Sirro kuondoa mianya ya rushwa Polisi huku akimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi, Mlowola kuchunguza mazingira ya uagizwaji magari hayo ya Polisi na kukwama.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top