Anaandika Benny Mwaipaja, Dodoma
SERIKALI imewalipa pensheni wafanyakazi 245 wa iliyokuwa Kampuni
ya Simu ya TTCL, chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kiasi cha shilingi
bilioni 12.7.
Hayo yamesemwa Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa
Ludewa Mhe. Deogratias Ngalawa, aliyetaka kufahamu, lini Serikali ingewalipa
wafanyakazi wa TTCL wa iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki madai ya pensheni
yao.
Dkt. Kijaji alisema kuwa malipo hayo yamefanyika kwa
wafanyakazi 245 ambao wamelipwa fedha zao kwa mkupuo ambapo kati yao wastaafu
54 walifariki dunia na malipo yao kulipwa warithi wao.
“Wastaafu 198 wanaendelea kulipwa malipo ya nyongeza ya
pensheni ya kila mwezi” alisema Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa malipo hayo yanafuatia uamuzi wa Mahakama Kuu katika
kesi namba 69/2005 ambapo wafanyakazi hao 254 waliishitaki Serikali kupinga
uamuzi wa kusitisha mfuko uliojulikana kama East Africa Non Contributory Pension Scheme.
“Katika Shauri hilo, Mahakama Kuu iliamua
kuwa, uamuzi wa Serikali kusitisha mfuko huo haukuwa sahihi kisheria na hivyo kuamua
wafanyakazi 254 waliokuwa katika shauri hilo walipwe madai yao ambayo
yalijumuisha malipo ya mkupuo, riba pamoja na pensheni yao ya kila mwezi”
aliongeza Dkt. Kijaji.
Alisema kuwa baada ya uamuzi huo wafanyakazi wengine 324 nao
walifungua kesi Makahama Kuu wakitaka walipwe pensheni kama wenzao walivyolipwa
wakati hawakuwa sehemu ya wafanyakazi waliofungua na kushinda kesi hapo awali.
“Mahakama Kuu iliamua kuwa, wafanyakazi waliofungua kesi ya
awali ndio walipwe madai yao, na kwamba deed of settlement iliyosajiliwa
Mahakamani ilihusisha wafanyakazi hao pekee” alifafanua Dkt. Kijaji.
Post a Comment
karibu kwa maoni