0
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho GamboMKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amewataka wakandarasi wataojenga hospitali au vituo vya afya kwenye wilaya mbalimbali za Mkoa wa Arusha kuhakikisha wanachora ramani ya ghorofa zaidi ya tano ili kutatua changamoto za uhaba wa maeneo.
Gambo aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha katika Kata ya Engutoto, wilayani Arusha. Alisema kutokana na ukosefu wa ardhi ni vyema sasa wakandarasi kwa kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri mbalimbali na wataalamu kuchora ramani ya ghorofa tano badala ya ghorofa moja.
Gambo alisema lengo la kuwa na ghorofa hizo ni kuondoa tatizo la uhaba wa ardhi na kusisitiza kuwa Mkoa wa Arusha umejipanga kuhakikisha kila wilaya inakuwa na hospitali ya wilaya na vituo vya afya ili kuondoa tatizo la upatikanaji wa huduma za afya.
“Nasisitiza kuwa Mkoa wa Arusha, ujenzi wa hospitali za wilaya lazima iwepo ramani ya ghorofa tano na kuendelea hata kama mtakwama fedha mtajenga kidogokidogo kwa sababu ya uhaba wa ardhi,” alisema.
Awali Mganga Mkuu wa Jiji la Arusha, Dk Simon Chacha alisema wananchi zaidi ya 80,000 wanatarajia kupata huduma za afya katika Hospitali ya Wilaya inayojengwa kwenye Kata ya Engutoto eneo la Block “D” lililopo Njiro Jijini Arusha.
Chacha alisema ujenzi huo wa hospitali ya wilaya utasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenye vituo mbalimbali vya afya vilivyopo Jijini Arusha na kuongeza kuwa mradi huo wa uwekaji wa jiwe la msingi ulianza kutekelezwa Desemba 5 mwaka huu na unatarajia kukamilika katika kipindi cha miezi saba.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top