Serikali ya India imeahidi kutoa mkopo
nafuu wa Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa
maji katika miji 17 nchini kupitia Benki ya Exim ya nchini humo.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na Balozi wa India hapa nchini Bw. Sandeep Arya.
Dkt. Mpango alieleza kuwa mradi huo
umelenga kumtua ndoo mama kichwani na kwamba mkopo huo utakapo patikana
utasaidia kutatua kero kubwa ya maji inayoikabili jamii hivyo kuchochea kwa kasi
ukuaji wa uchumi.
“Tuko katika mazungumzo ya kukamilisha
upatikanaji wa mkopo huo ikiwemo kuangalia namna ya kushughulikia madai ya
Benki ya Exim ambayo inataka hata kampuni itakayotekeleza mradi huo isamehewe
kodi zote zikiwemo zinazopaswa kulipwa na wafanyakazi wake” alieleza Dkt.
Mpango
Alibainisha kuwa licha ya kwamba jambo
hilo ni gumu kisheria lakini kutokana na umuhimu wa suala hilo la maji, Serikali
italipatia ufumbuzi hivi karibuni ili
mradi huo uweze kuanza mara moja.
Dkt. Mpango alitambua mchango mkubwa wa
Serikali ya India katika kutatua changamoto ya maji kwa watanzania ambapo
amesema kuwa inchi hiyo inatatekeleza mradi mkubwa wa maji wa Ziwa
Victoria-Shinyanga hadi Tabora.
Dkt. Mpango aliiomba Serikali ya India
iendelee kuisaidia Tanzania katika Nyanja za utaalamu wa teknolojia ya habari
na mawasiliano-TEHAMA ili kupata watu wenye ujuzi utakao saidia kuchochea kasi ya maendeleo ya Sekta ya
Viwanda nchini.
Dkt. Mpango alisema kuwa nchi ya India imepiga hatua kubwa katika
masuala ya TEHEMA hivyo ni vema ikawekeza kwenye eneo hilo katika Taasisi za Elimu hapa nchini ili
kuweza kuwapatia ujuzi idadi kubwa ya watu watakao kwenda kusukuma gurudumu la
maendeleo hasa ya ukuaji wa viwanda.
“Bila kuwa na watu wenye ujuzi katika
kada mbalimbali hasa TEHAMA hatuwezi kuwa na nchi yenye uchumi wa viwanda”,
aliongeza Dkt. Mpango.
Aliyataja maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji kuwa ni pamoja
na Sekta ya Kilimo ambapo Tanzania inahitaji kuwa na viwanda vitakavyoongeza
thamani ya mazao na pia kuwa na zana bora za kilimo kama utumiaji wa Trekta
badala ya kutumia jembe la mkono.
Maeneo mengine ni sekta ya utalii,
afya, uendelezaji wa ujuzi kupitia fani nyeti za udaktari ama utaalamu nyeti ya
tiba ikiwemo magonjwa ya moyo na figo, ambayo India imepiga hatua kubwa.
“Pia ujuzi wa Wahandisi katika Sekta ya
Maji unahitajika ili kutoa huduma ya maji kwa weledi kwa jamii kwa kuwa ni moja
ya hitaji muhimu kwa maendeleo, hata hivyo zipo sekta nyingine za uwekezaji kama
Utalii na Uvuvi hasa katika kina kirefu ambao unahitaji
zana bora” aliongeza Dkt. Mpango
Kwa upande wake Balozi wa India nchini
Tanzania Bw. Sandeep Arya, amesema nchi
yake inania ya kuwekeza katika Kilimo, Nishati ya Umeme hasa wa Jua na kusaidia
katika mpango wa ujenzi wa Mji wa Dodoma pamoja na ujenzi wa Reli na Barabara.
Amesema Tanzania na India zinauhusiano
wa muda mrefu hivyo nchi yake itaendelea kuwekeza Tanzania katika Nyanja
mbalimbali ili kuendeleza ushirikiano wenye tija kwa wananchi wa pande hizo
mbili.
Post a Comment
karibu kwa maoni