0
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 10 Desemba, 2017 ametia saini nyaraka za msamaha alioutoa jana kwa wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.

Mhe. Rais Magufuli ametia saini nyaraka hizo Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma na kuwapongeza Jeshi la Magereza kwa kazi nzuri wanayoifanya kurekebisha tabia za wafungwa wa makosa mbalimbali.

Mhe. Rais Magufuli amesisitiza kuwa pamoja na kutolewa kwa msamaha huo, vyombo vya dola viendelee kusimamia sheria, na kwa Jeshi la Magereza amelitaka kuhakikisha linawatumia wafungwa kuzalisha mali ikiwemo kuzalisha mazao ya kilimo na kufanya kazi za ujenzi.

“Nimeona nitumie kifungu hiki cha Katiba (Ibara ya 45 {1}) ambacho nilipewa na Watanzania, ingawa kilikuwa hakijawahi kutumika, unajua mtu ambaye alihukumiwa kunyongwa halafu baadaye anaachiwa, ni kitu kinashangaza kwa sababu hakijawahi kutokea, lakini nimeona nifanye hivyo kwa ajili ya Watanzania”

“Mimi nikuombe tu, muendelee kusimamia wajibu wenu na kusimamia sheria, mtu anayehukumiwa kufungwa afungwe kweli, na nilishatoa wito kwa magereza, pasiwepo wafungwa wa kukaa tu na kupumzika, wafanye kazi, kufungwa sio kustarehe” Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Magereza Dkt. Juma Malewa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kutoa msamaha huo wa kihistoria na kubainisha kuwa wafungwa na Maafisa Magereza wameipongeza hatua hiyo, ambayo itasaidia kuwatia moyo wafungwa wanaorekebishwa tabia katika magereza mbalimbali nchini.

Kamishna Jenerali Malewa amesema wafungwa waliopatiwa msamaha wa kuachiwa huru, waliruhusiwa kutoka magerezani tangu jana na Maafisa Magereza wamewaasa kwenda kuonesha mfano bora kwenye jamii watakakwenda kuishi.

Katika hatua nyingine Mhe. Rais Magufuli amelipongeza Jeshi la Magereza kwa kutekeleza agizo lake la kutengeneza viatu kwa ajili ya askari wake badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi.

Jeshi la Magereza linazalisha jozi 150 za viatu kwa siku katika kiwanda chake cha Karanga kilichopo Moshi Mkoani Kilimanjaro, na kwa kushirikiana na mfuko wa hifadhi ya jamii wa PPF limeanza kuboresha kiwanda hicho ili kufikia uzalishaji wa jozi 450 kwa siku.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma

10 Desemba, 2017

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top