Anaandika Benny Mwaipaja-DODOMA
Dhana kuu ya mkutano huo wa COBAT
uliowashirikisha wadau mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ni "Mitaji
na Mpango wa Kuziunganisha Benki za Wananchi Tanzania", ambayo ni dhana
mpya.
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa, ameiagiza Benki Kuu ya Tanzania BOT kuzifutia leseni benki
zote za biashara pamoja na benki za wananchi zitakazoshindwa kukidhi vigezo vya
kuendesha shughuli za kibenki nchini.
Ametoa
agizo hilo mjini Dodoma katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Waziri wa
Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, wakati akifungua Mkutano Maalum wa Wadau
wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT).
“kwa taarifa niliyonayo hadi sasa baadhi ya benki
hazijatimiza matakwa ya kisheria ya kuwa na mtaji wa kutosha, hali ambayo
haiwezi kuachwa iendelea hata kidogo, kwani haiimarishi sekta ya fedha na
haiwasaidii wananchi kuendelea kiuchumi” alisema Waziri Kassim Majaliwa katika
hotuba hiyo
Alisema Benki Kuu ilitoa muda hadi mwishoni mwa Desemba
2017, benki za wananchi ziweze kuongeza mtaji na kwamba muda huo hautaongezwa
na wala Serikali haitatoa mtaji kwa benki hizo.
“Serikali kupitia Benki Kuu ya
Tanzania haitasita kuifungia benki yoyote na kufuta leseni yake ya biashara
pindi itakapobaini inavunja sheria, ikiwa ni pamoja na kuwa na upungufu mkubwa
wa mtaji na ukwasi ambao unahatarisha usalama wa sekta ya fedha na amana za
wateja kama tulivyofanya kwa Mbinga Community Bank PLC kuanzia tarehe 12/5/2017”
alisema Dkt. Mpango kwa niaba ya Waziri Mkuu.
Maagizo hayo yamekuja siku moja
baada ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kuiagiza Wizara ya Fedha na
Mipango wakati akifungua tawi kuu la Benki ya CRDB mjini Dodoma, kuhakikisha
kuwa Benki Kuu ya Tanzania-BOT, inazifuta benki zote zinazoshindwa kujiendesha kibiashara
hata kama zinamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100.
Alisema Serikali inafanya jitihada
mbalimbali ili kuhakikisha benki za wananchi zinaimarika zikiwemo kuruhusiwa
kuanzisha mifumo ya ushirikiano katika Nyanja ya Mfumo wa Mawasiliano na Habari
(ICT), Idara za Ukaguzi wa Ndani (Internal Audit Services), kupunguza wingi wa
idara na kuwa na idara tatu (3) tu muhimu, kuruhusiwa kuungana (Federation), ambazo
zitapunguza gharama za uendeshaji wa benki za wananchi na kuleta ufanisi katika
kutoa huduma.
“Napenda kusisitiza kuwa sekta ya
benki ni muhimu sana kwa uhai na ukuaji wa uchumi kama ilivyo damu kwa mwili wa binadamu
na kutokana na umuhimu wake huo, sekta hii ni kati ya sekta chache
zinazosimamiwa kwa karibu sana ili
kulinda amana za wateja pamoja na kuhakikisha uhimilivu wa mfumo mzima wa sekta
ya fedha na mwenendo wa uchumi wa Taifa” aliongeza Dkt. Mpango
Kwa upande wake Afisa Mtendaji
Mkuu wa Jumuiya ya Benki za Wananchi Tanzania (COBAT) Bw. Rukwaro Senkoro, alisema
hadi kufikia Juni, 2017, Benki za Wananchi nchini zilikuwa na wateja
zaidi ya milioni 1.4, wateja wa vikundi zaidi ya 10,000, Matawi 12, Vituo 59, na
wanahisa 66,492.
“Benki hizo zina amana zenye thamani ya shs bilioni 74.2, zimetoa mikopo
ya sh. bilioni 56.8, na jumla ya mali zenye thamani ya shs. bilioni 92.3”
Alisema Bw. Senkoro
Hata hivyo, kutokana na Utafiti wa Matumizi ya Huduma za Kifedha
uliofanyika mwaka 2017 umebaini kuwa asilimia 28 ya wananchi bado hawapati
huduma za kifedha hapa nchini hususan vijijini na kutaja changamoto ya ukosefu
wa mitaji ya benki hizo kukwaza sekta hiyo.
Post a Comment
karibu kwa maoni