0
Wizara ya Fedha na Mipango -WFM
VYAMA vya kuweka na kukopa fedha (SACCOS) vimekuwa ni suluhisho la mikopo chechefu (non performing loans) kwa kutoa riba nafuu ukilinganisha na taasisi zingine za kifedha kama benki za kibiashara. 
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Hazina, Bw. Eligius Mwankenja alipokua akifungua mkutano wa mwaka wa Chama hicho Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa chama hicho kinatoa riba ya kiasi cha asilimia 6.5 hadi 9 ilihali Taasisi nyingi za Fedha zikiwemo Benki hutoa riba ya zaidi ya asilimia 20 jambo linalochangia ongezeko la Mikopo chechefu.
“Hazina Saccos kwa kutambua kuwa watu wanaokopa wengi hawana dhamana kama nyumba, ardhi na vingine, imeamua kutumia kigezo cha kubakiwa na 1/3 ya mshahara kama kigezo cha kupatiwa mkopo wenye riba nafuu” alifafanua Bw. Mwankenja.
Kwa upande wake Meneja wa Hazina Saccos ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Chama hicho Bw. Festo Mwaipaja, alisema kuwa chama hicho kipo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango na kinahudumia Wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake.
Kutokana na uwezo mkubwa wa chama hicho kujiendesha kimetoa ajira kwa wafanyakazi 11 ambao wanatekeleza majukumu ya kila siku ya chama na pia kimekuwa kikipata faida na kutoa kodi kwa Serikali hivyo kuchangia katika pato la Taifa kwa ujumla.
Aidha Chama kinatarajia kufungua mradi mkubwa wa Kitega Uchumi maeneo ya Njedengwa Mkoani Dodoma kwenye eneo lililotengwa kwa ajili yauwekezaji zikiwa ni juhudi za kukuza mtaji na kuchangia maendeleo.
“Jambo linalo vutia katika chama hichi ni kuwa Mwanachama wa Hazina Saccos anaweza kuchangia Sh. 20,000 kila mwezi kwa muda wa miezi mitatu lakini akawa na uwezo wa kukopa zaidi Sh. milioni moja hadi milioni tatu pia tunatoa mikopo ya biashara kwa wanachama jambo ambalo ni suluhisho la mitaji hivyo kuchangia kukuza uchumi wa nchi”. alieleza Bw. Mwaipaja.
Vilevile kimetoa viwanja kwa bei nafuu katika maeneo ya Kigamboni kwa Sh. 6500 kwa mita ya mraba, Chasimba kwa Sh. 4000, Kiluvya Sh. 7500 na sasa kinatarajia kutoa viwanja Mkoani Dodoma katika Maeneo ya Ihumwa, Ngaroni na Nzuguni B.
Chama cha Hazina Saccos kilianzishwa mwa 1973 kikiwa na wanachama 250 lakini kwa sasa Chama hicho kina wanachama hai 5045.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top