0
Mahakama ya Rufaa imesema hakuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido iliyopo mahakamani hapo.

Mahakama imetoa kauli hiyo wakati Chadema ikiilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo kwa madai kwamba kuna kesi mahakamani hapo.

Uchaguzi huo mdogo ulifanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa Longido kwa tiketi ya Chadema, Onesmo ole Nangole ushindi wake kutenguliwa na Mahakama Kuu.

Mara kadhaa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Ole Nangole wamekaririwa na vyombo vya habari wakidai kwamba kuna rufaa katika Mahakama ya Rufani.

Viongozi hao wamekuwa wakiilalamikia NEC kuwa iliendesha uchaguzi mdogo katika jimbo hilo wakati rufaa ya kupinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomvua ubunge Ole Nangole ikiwa haijatolewa uamuzi.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa imesema uchaguzi mdogo uliofanyika Longido ulikuwa halali kwa kuwa hakuna rufaa yoyote iliyoko mahakamani hapo.

Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu amesema hakuna rufaa yoyote kupinga hukumu ya uchaguzi wa Longido iliyoko mahakamani hapo, bali kuna maombi.

“Hapa hatuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido, bali kuna maombi ya kuongezwa muda wa kuwasilisha ‘notice of appeal’ (taarifa ya kusudio la kukata rufaa). Walileta notice of appeal lakini ikatupiliwa mbali, sasa wanaomba muda ili waiwasilishe tena,” alisema na kuongeza:

“Maombi si rufaa, kwa hiyo haya maombi yasingeweza kusimamisha shughuli za uchaguzi.”

Kwa mujibu wa ratiba ya vikao vya Mahakama ya Rufaa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji Jacob Mwambegele Februari 5.

Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, mwombaji kupitia kwa mawakili wake atalazimika kutoa sababu za kuiridhisha Mahakama ni kwa nini alichelewa kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Ikiwa Mahakama haitaridhika na sababu zake, itatupilia mbali maombi hayo lakini ikiridhika nazo itamruhusu kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.

Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, atasubiri kupata kumbukumbu za rufaa, yaani nyaraka zitakazohusika kwenye rufaa yake, ikiwamo hukumu anayoilalamikia, mwenendo wa kesi ya msingi na vielelezo vilivyotumika.

Akipata nyaraka hizo, ndipo atakapowasilisha rufaa kamili, yaani sababu za kwa nini anapinga hukumu iliyomvua ubunge wa jimbo hilo, na upande wa pili (wajibu rufaa) nao utawasilisha hoja zake na baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote ndipo itatoa hukumu.

Ole Nangole alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Juni 29, 2016 kutokana na kesi ya uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya CCM, Dk Steven Kiruswa akipinga ushindi wake.

Baada ya Mahakama kumvua ubunge, Ole Nangole kupitia mawakili John Materu na Dancan Oola aliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Hata hivyo, taarifa hiyo ya kusudio la kukata rufaa ilitupiliwa mbali na Mahakama kutokana na kasoro za kisheria.

Baada ya kutupiliwa mbali, kwa kuwa muda wa kisheria wa siku 14 za kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ulikuwa umeshaisha, waliwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha taarifa hiyo.

Maombi hayo pia yalitupiliwa mbali na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ndipo wakapeleka maombi Mahakama ya Rufani.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top