0
Mvua zinazoendelea kunyesha nchini zimesababisha madhara katika Mikoa ya Arusha na Manyara.

Katika Mkoa wa Arusha, mvua hizo jana zilisababisha shughuli za maendeleo katika Barabara Kuu ya Arusha kwenda Karatu, kusimama kwa muda, baada ya kingo za daraja linalounganisha Mji wa Mto wa Mbu na Makuyuni kusombwa na mafuriko.

Kutokana na hali hiyo, abiria wanaotoka na kwenda mkoani Mara, watalii wanaotembelea Hifadhi za Manyara, Serengeti, Ngorongoro pamoja na wananchi mbalimbali, walijikuta katika wakati mgumu wa kuendelea na shughuli zao za kila siku kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Kukatika kwa daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu cha shughuli za maendeleo, kulisababishwa na mvua kubwa iliyonyesha maeneo ya milimani, wilayani Monduli na kusababisha magari zaidi ya 300 kushindwa kupita kwa wakati.

Akizungumzia athari hizo kwa njia simu, Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Arusha, Mgeni Mwanga alisema baada ya uharibufu wa barabara hiyo, wamefanikiwa kuweka kifusi katika eneo hilo na magari yalianza kupita, kuanzia jana saa sita mchana.

“Usiulize ukiwa mbali, njoo hapa ‘site’ uone kwa macho yako kama kweli kuna daraja limesombwa na mafuriko kama unavyouliza.

“Kimsingi, daraja halikukatika ila kingo zake ndizo zimemegwa na maji baada ya maji kujaa kupita kiasi.

“Yaani, hivi ninavyozungumza na wewe, tunamalizia kujaza kifusi na magari yote yalishaanza kupita na kuendelea na safari,” alisema Mwanga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Isack Joseph, alisema kukatika kwa daraja hilo kulisababisha madhara kwa wananchi wilayani kwake.

“Maeneo mengi wilayani Monduli yalikuwa na mvua kubwa sana jana usiku na kwa kuwa wilaya ina maeneo yenye milima, maji yaliteremka kwa wingi kuelekea chini.

“Kazi ya kutafuta njia mbadala ili kuruhusu magari na watumia barabara waendelee na shughuli zao, zinafanywa kwa ushirikiano wa TANROADS na halmashauri,” alisema Joseph.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Iddi Kimanta alisema jitihada za kurudisha usafiri katika hali ya kawaida zilifanikiwa na magari kuanza kupita.

Pamoja na hayo, Kimanta alisema Serikali ya Wilaya ya Monduli inaendelea kufuatilia madhara ya mvua hizo na itatoa msaada kwa waathirika pindi utakapohitajika.

Post a Comment

karibu kwa maoni

 
Top