Lissu
ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS),
alipelekwa Ubelgiji Januari 7, mwaka huu, akitokea Hospitali ya Nairobi
nchini Kenya alipokuwa akipatiwa matibabu tangu Septemba 7, mwaka jana.
Mbunge
huyo aliumia vibaya baada ya kushambuliwa kwa risasi 32 na watu
wasiojulikana nyumbani kwake mjini Dodoma Septemba 7, mwaka jana, tano
kati ya hizo zikimpata katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Vinceti
Mghwai, ambaye ni mdogo wa Lissu, alisema jana kuwa Lissu ameanza
kutembea mwenyewe kwa kutumia magongo na kujipatia huduma mbalimbali
ikiwemo kwenda kuoga bila msaada wa mtu mwingine.
"Tunamshukuru
Mungu sana, Lissu anaendelea vizuri... tangu ameanza kupatiwa matibabu
na mazoezi ya viungo tunaona mabadiliko makubwa mno," alisema na kueleza
zaidi:
"Maendeleo
ni makubwa sana, kuna vitu alikuwa hawezi kuvifanya lakini sasa anaweza
kuvifanya mwenyewe kama kuoga. Siku za nyuma alikuwa akipelekwa
maliwatoni lakini sasa hivi anatembea na magongo mwenyewe kwa kukanyagia
mguu chini.
"Anakula mwenyewe.Tunaamini atatengamaa mapema zaidi, (na) haya kwetu ni maendeleo makubwa."
Mghwai
alisema Lissu anapata muda mwingi wa kupumzika na huenda hiyo ndiyo
ikawa sababu kubwa ya yeye kuendelea kupona haraka kutokana na kupatiwa
matibabu na bila usumbufu wowote.
Alisema
Lissu anapata matibabu katika mazingira tulivu tofauti na alipokuwa
Hospitali ya Nairobi ambako alikuwa akisumbuliwa na makundi ya watu
waliokuwa wakienda kumjulia hali.
"Kwa
sasa ana muda wa kutosha kufanyiwa matibabu ya mazoezi, madaktari
wanamfanyia mazoezi muda wote kwa sababu hakuna watu wanaokwenda kumuona
na ndiyo sababu anaendelea kupona haraka," alisema Mghwai.
"Ubelgiji
muda wote yuko na madaktari akipatiwa matibabu hasa mazoezi ya
viungo... huku ni kazi kazi tu. Na madaktari waliahidi kufanya kazi.
"Kule
Nairobi wakati mwingine alikuwa akiwaambia madaktari wamuache pale
anaposikia maumivu wakati wa mazoezi lakini sasa hakuna kitu kama hicho
na wamemwambia avumilie apone."
Kuhusu
risasi iliyobakia kwenye nyonga, Mghwai alisema madaktari wa Ubelgiji
hawataitoa na wataiacha kwa sababu walishaeleza kuwa haiwezi kuwa na
madhara kwake kiafya.
"Kule
Ubelgiji kazi kubwa ni kumfanyisha mazoezi ili sasa aweze kurejea
katika hali yake na ndicho ambacho wanaendelea nacho na kwa kweli
tumeanza kuona maendeleo makubwa."
Kuhusu
gharama za matibabu, Mghwai alisema, zaidi ya Sh. milioni 100
zinatumika kila mwezi kwa ajili ya kumtibu na kwamba hadi sasa Bunge
halijatoa fedha na familia inafuatilia lakini wamekuwa wakizungushwa
huku na kule.
Alisema
fedha zinazotumika kwa ajili ya matibabu yake ni zile zilizochangwa na
wadau mbalimbali na wamekuwa wakifanya harambee kadhaa za kuchangia.
"Gharama
ni kubwa sana kwa mwezi analipia zaidi ya milioni 100 katika hospitali
hiyo na kama atakaa miezi miwili tutatumia zaidi ya milioni 200 na hizi
ni fedha za matibabu pekee," alisema Mghwai.
Alieleza
zaidi kuwa fedha zilizochangwa hazitoshi kumtibu Lissu na kwamba kwa
sasa wadau wamesitisha kutoa michango baada ya tetesi kuwa serikali
inagharamia matibabu yake.
Alisema familia inaendelea na juhudi za kuchangisha fedha zaidi ili kukamilisha matibabu yake.
"Tunaamini hakuna kitakachoharibika kwa sababu tumeshaweza kumponya tunaamini atakuwa mzima."
Alisema
gharama kamili za matibabu na fedha zilizopatikana kwa ajili ya
matibabu ya Lissu zinaweza kuzungumzwa katika vikao vya makubaliano na
si yeye peke yake kuzungumzia.
Lissu
ambaye Januari 6 alizungumza na waandishi wa habari akiwa nje ya
Hospitali ya Nairobi, ikiwa ni siku moja kabla ya kusafiri kuelekea
nchini Ubelgiji, alieleza kuwa alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 20 na
16 zilimjeruhi maeneo mbalimbali ya miguu, mikononi na kwenye nyonga.
Lissu
alisema kutokana na shambulio hilo alifanyiwa operesheni 17
zilizofanikisha kuondoa risasi saba zilizoingia mwilini huku risasi moja
ikisalia.
Wataalam
wa afya walimshauri kuiacha risasi hiyo iliyopo kwenye nyonga wakisema
kuwa inaweza kuleta madhara zaidi kama watajaribu kuitoa.
Post a Comment
karibu kwa maoni